Gharama ya kustaafu: Rais wa Burundi Kupewa shilingi milioni 53 kuondoka madarakani

Nkurunziza
Nkurunziza
  Bunge la Burundi limepitisha hoja ya kumlipa rais wa taifa hilo  Pierre Nkurunziza  shilingi milioni 53 pamoja na kumjengea jumba la kifahari atakapoondoka madarakani.

Mswada wa sheria uliowasilishwa mbele ya baraza la mawaziri ili kuidhinishwa pia unapendekeza rais huyo kulipwa mshahara maisha yake yote. Pendekezo jingine ni kumpa wadhfa wa ‘Kiongozi mkuu’ wa nchi atakapoondoka afisini mwezi Mei mwaka huu. Burundi ilitumbukia katika mgogoro wa kisiasa mwaka wa 2015 wakati Nkurunziza alipowania muhula wa tatu .

Hatua hiyo ilizua maandamano yaliyokuwa na vurugu  na kusababisha mashambulizi ya kulipiza kisasi kutoka kwa wafuasi wa rais huyo. Mwaka jana Umoja wa mataifa uliishtumu serikali ya Burundi kwa ukiukaji wa haki za binadamu, ikiwemo kukamatwa kwa watu bila hatia, mauaji ya kiholela, mateso na dhulma za kimapenzi. Burundi imeyakana madai hayo na kuyataja kama ‘uongo’.

Mwaka jana Burundi ilipiga marufuku shirika la habari la BBC kuhudumu nchini humo kwa kutayarisha makala yaliodaiwa kuiharibia sifa nchi hiyo .