Mlikutania wapi? Fahamu jinsi watu walivyokutana na wapenzi wao

Ndoa 2
Ndoa 2
  Kila mtu ana stori  ya kuvutia na hata kutoa machozi kuhusu jinsi alivyokutana na mpenzi wake na wengine wakikupa  masimulizi ya jinsi walivyokutana, basi utajawa hisia lakini hebu soma kuhusu sehemu na hali mbali mbali nyingine za kipekee za jinsi wapenzi hao walivuokutana …

  1. Matatu ‘mates’

Peris na  Edwin walikuwa  abiria katika matatu moja  kutoka Lang'ata  kwenda mjini Nairobi wakati mazungumzo ambayo yangewapeleka katika safari ya ndoa yao yalipoanza. Edwin  bila kukusudia aliangusha noti ya shilingi mia mbili na  Peris aliyekuwa ameketi kando yake aliiona na kumuambia kwamba alikuwa ameanguisha pesa. Edwin alipoangalia, kweli alipata  noti hiyo na kumshukuru mwenzake kwa  utu wake na ukarimu wa kuweza kumjulisha.

Wakiendelea na safari Edwin akaendelea kusema na Yule mwanadada akashangaa mbona hajanyamaza ile aichukue ile noti? Peris alimuambia alivyokuzwa hangeweza kuchukua pesa ambazo sio zake  na hata akamfanyia utani akisema labda huenda hiyo noti ndio aliokuwa nayo  mfukuni Edwin, walicheka wote wakati Edwin  alipokubali kwamba ni kweli hakuwa na pesa za ziada isipokuwa ile noti. Safari ilipokaribia kufika tamatai,walipjipata wakibadilisha nambari za simu na wakaanza kukutana mara kwa mara. Muda sio mrefu Edwin na Peris walikuuza urafiki mzito uliotumbukia  kuwa penzi na kuzaa ndoa yao.

2.Polisi na Muuguzi

Stori ya walivyokutana Philip na Esther ni kama  masimulizi ya filamu ya nollywood. Hebu fikiria kukutana na mpenzi wako mtarajiwa katika hali za kikazi bila hata kufahamu kwamba miaka michache baadaye mtakuwa mkiamka kutoka kitanda kimoja kila siku. Philip alikuwa afisa wa polisi mtaani Mukuru, Nairobi na siku moja akipiga doria na wenzake katika mtaa huo wa mabanda ,wakapatana na majambazi waliokuwa wamejihami.

Agizo la polisi kwa majambazi kusimama lilisababisha ufyatulianaji wa risasi  na matokeo yake yakawa Philip kujeruhiwa kwa kupigwa risasi pajani. Alikimbizwa katika zahanati moja mtaani humo iliyokuwa ikihudumu  saa 24. Katika zahanati hiyo, muuguzi  Esther ndiye aliyekuwa katika zamu ya usiku na akampa huduma ya kwanza  Philip kabla ya polisi huyo kuhamishwa  hadi  katika hospitali  Kuu ya Kenyatta. Baada  ya kupona  Philip alichukua hatua ya kwenda katika kliniki ili kumshukuru  muuguzi aliyempa huduma ya kwanza na kuokoa maisha yake. Alipofika, Philip alivutiwa na urembo wa yule muuguzi na pale pale alijikatia kauli moyoni kwamba  lazima  angemshawishi awe mpenzi wake. Safari ya kuuteka moyo wake ilianzania pale na miaka miwili baadaye, walikuwa mume na mke .

3.Good Samaritan

Andrew  na Nancy walikutana kwa njia ya kuhuzunuisha na  baadaye ikawa ni kicheko kwao  wote wakikumbuka jinsi walivyokutana.  Nancy alikuwa akienda kumtembelea jamaa yake Eldoret  wakati alipoibiwa  kila kitu na kuachwa   bila hata nauli  na alichobakishwa nacho ni nguo zake mwili na jina lake akilini. Katika steji ya magari giza likiingia Nancy alikuwa amelia hadi koo likakauka na sauti hakuwa nayo. Watu walikuwa wakimpita tu wengine wakifikiri labdaa kaachwa na mumewe au amepagawa ila hakuwa katika hali nzuri kuweza kueleza yaliomsibu .

Andrew alikiharakisha kwenda zake nyumbani , ndiye aliyekuwa na huruma ya kumsongea  pale na kumsalimia ili kumuuliza mbona alikuwa analia na  kuonekana kupotea . Nancy alipata ujasiri wa kusimualia yaliomtokea na Andrew akaahidi kumpa mahali pa kulala usiku ule mtaani Langas ili kesho amsaidie kupata jamaa zake.  keshoye walionana vizuri sasa na wakazungumza na muda si muda ikawa kweli damu yao imeingiana. Mawasiliano kati yao yaliendelea hata wakati Nancy alipofaulu kumpata jamaa yake na baadaye ikawa ni bayana kwamba waliamua kuoana . Kumbukumbu za siku hiyo zinawapa machozi ya  furaha  kweli .

  1. Mtandaoni (facebook,insta,Tinder)

Umesikia kuhusu wapenzi waliokutana kupitia mitandao ya kijamii  ingawaje kumekuwa na  woga siku hizi kwa watu kukutana na kuchukulia kwa uzito uhusiano unaoanzia mtandaoni.  Mtangazaji wa runinga  Jackie Matubia maajuzi ameisimulia Radio Jambo jinsi alivyokutana na mume wake kupitia instagram .Ingawaje baadaye walitengana, Ndoa yao iliweza kuwapa mtoto. Iwapo labda hapengetokea tofauti kati yao, mtandao bado ni sehemu unayoweza kukutana na mke au mumeo.

Molly na   Charles walikutana kupitia facebook  na mwanzoni rafiki zao hawakuamini kwamba kweli wapenzi wale walikutana mtandaoni. Wengi hata hivyo walikuwa  wamesema uhusiano wao ungekatika lakini ole wao, Molly na Charles walifunga ndoa. Yote yalianzia katika posti ya picha ambayo  Charles aliiweka facebook akiwa   juu ya mlima Kilimanjaro. Molly ‘aliilike’ ile picha na muda si mfupi Charles alitaka kujua ni nani Yule ambaye amezipenda picha zake zote za Kilimanjaro?  Kwa ujasiri alitumbukia katika inbox yake kujitambulisha na kutaka kumjua Molly na pale Molly naye akamuambia jinsi anavyotamani sana siku moja pia kwenda kukwea mlima Kilimanjaro.Pale pale wakaanza mawasiliano ya kila mara na baadaye waliweza kukutana  ana kwa ana baada ya mwaka mmoja. Ilipangwa safari nyingine ya kwenda Mlima Longonot ambapo waliandamana na rafiki zao na muda mfupi baadaye walikuwa wapenzi. Mwaka mwingine mmoja  ilifanywa ndoa na hivyo ndivyo facebook ilivyowageuza marafiki wa mtandao kuwa mume na mke .

  1. Hakuna matatu kuingia CBD,Nairobi

Mwaka wa 2018, kaunti ya Nairobi iliwakataza wahudumu wa matatu kuingia hadi katikati mwa jiji. Matatu zilianza kuwaacha abiria nje ya jiji na wengi walianza kutembea kwa miguu kutoka vituo vya magari yao hadi CBD. Katika hali hiyo ndivyo Rebecca na  Joseph walivyopatana.  Ni  Kinaya  kwamba  uchungu wa kutembea kutoka Ngara, fig tree hadi  Teleposta Towers  kulimletea raha Jose wakati alipokuwa akitembea  kutoka eneo hilo la Ngara hadi CBD kwa siku mbili. Siku ya tatu aligundua kwamba alikuwa akipanda gari moja kutoka mtaa wake na mwanadada  Fulani aliyekuwa na macho mazuri na rangi ya kupendeza. Alikuwa na uhakika kwamba ni Yule msichana aliyekuwa akishuka kutoka matatu alioabiri na kutembea pia kama yeye hadi CBD.

Siku ya nne  Jose  aliamua kutupa chambo ili kujaribu  bahati yake na wakaanza gumzo na yule mwanadada. Wakaanza kungojana kila wakati wakitokea mtaani Kinoo na kutembea kwa pamoja  hadi katikakati mwa jiji. Baadaye wasipoenda kazini walianza kupigiana simu Jumapili kwenda kanisani kwa sababu kwa bahati nzuri pia walikuwa wa dhehebu moja na hivyo ndivyo mtu na mkewe walivyoanza maisha ya ndoa .

6. Sehemu mbali mbali

Huwezi kujua utakutana vipi na mtu ambaye utamuoa au  atakaye kuoa. Mola tu ndiye anayeijua safari hiyo. Kuna waliokutana shuleni, kazini, sokoni, kanisani na hata katika baa na maeneo ya burudani. Kuna hata watu waliokutana na wapenzi wao njiani wakiwa safarini. Kuna visa vya mgonjwa aliyependana na daktari wake, mwalimu aliyempenda mwanafunzi wake, mwajiri aliyempenda  mfanyikazi wake na hata  mtoto wa mdosi aliyempenda mfanyikazi wa nyumbani.

Kuna hata kisa cha mtu aliyepatana na mke wake katika seli! Polisi waliwakamata wasichana wengi katika karamu moja ya birthday na baada ya kila  msichana kutolewa seli na jamaa zake kuna mmoja aliyebaki mle ndani. Afisa mmoja wa polisi alimhurumia na kumsaidia aachiliwe huru. Baadaye walianza uhusiano ambao uligeuka na kuwa ndoa ! Pia kuna kondakta wa matatu aliyempenda abiria wake au dereva  wa teksi aliyempenda mteja wake wa kila mara. Kuna kisa cha    mnunuzi kupendana na muuzaji wa bidhaa sokoni na hata kuna visa vingi  vya wasichana wanaohudumu katika hoteli kuolewa na baadhi ya wateja ambao huja pale kwa chakula. Kuna hata watu waliokutana viwanjani katika mechi za soka au hata katika gym wanakofanyia mazoezi.

Hebu tuambie hali na sehemu zisizotarajiwa  ambazo watu walikutana  na kuanza uhusuiano ulioimarika na kuishia katika ndoa.Ulikutana vipi na mpenzi au mwenzako?