Kabla ya masimulizi ya Jane Mbithi mwenye umri wa miaka 32 sasa kuibuka, wengi nchini hawana ufahamu iwapo kuna utamaduni kama huo. Jiwe hutiwa motoni kama kaaa kisha kupitishwa juu ya matiti kwa lango la kuyapunguza. Jane alifanyiwa utataribu huo miaka 18 iliyopita na shangazi yake ambaye alikuwa Mtawa(Nun) na alikuwa akiishi Cameroun wakati huo . Alipokuja nyumbani kwa likizo alimpata Jane akiwa ameanza kubaleghe na matiti yake yameanza kujitokeza, yakionekana kupitia nguo yake. Shangazi yake hakufurahia hilo na mara moja akamuambia mamake jane kuhusu hatari ya mwanawe kubakwa na wanaume na hivyo basi kuliwa na haja ya kuyapunguza matiti yake. Mamake alishangaa hilo litafanywaje lakini shangazi yake kwa ajili ya kuwa mtawa aliheshimiwa sana pale bomani na kila alichosema kilikuwa sheria. Alieleza jinsi utaratibu huo utakavyofanywa na muda sio mrefu, kila jane alikuwa akivumilia takriban dakika 20 za uchungu wakati jiwe la moto lilipokuwa likiwekwa kifuani mwake ili kupunguza kiasi cha matiti yake .
Wenzake shuleni walishangaa mbona alikuwa akilia wakati wote na kushika kifua chacke kwa uchungu. Wengine kama rafiki yake wa karibu Stella alishangaa mbona hawakuwa wakioga pamoja kama awali bila kujua kwamba Jane alikuwa akificha alama katika kifua chake na kupungua kwa matiti yake kwa ajili ya uovu aliokuwa akifanyiwa na shangazi yake kutumia mila aliotoa Cameroun .
Alipokuwa msichana mkubwa kujiunga na chuo kikuu, Jane alijipata na matatizo ya kujiamini kwa sababu alijiona na kujihisi tofauti kama wasichana wenzake. Wengine walikuwa wakimfanyia mzaha kwa kumuita ‘mvulana’ kwa sababu ya kukosa matiti bila kujua masaibu aliyopitia . Jane hakuweza kumchukulia hatua yoyote shangazi yake kwa sababu uamuzi huo pia ungemuingiza taabani mamake ambaye alikuwa amekubali afanyiwe utaratibu huo . Walimuambia wakati huo kwamba kila wanachofanya ni kwa manufaa yake bila kujua athari za kitendo hicho katika maisha yake ya baadaye .
Nchini Cameroun ambako utamaduni huo umekithiri, serikali na mashirika mbalimbali ya haki za binadamu yanapambana na uovu huo ili kuzuia mateso kwa maelfu ya wasichana. Kupiga matiti pasi ni zimwi kama utamaduni wa kuwakeketa wasichana katika baadhi ya jamii za humu nchini. Athari za kitendo hicho kwa Jane hazitaisha hivi karibuni na zinamuathiri hadi wakati huu katika maisha yake ya utu uzima .