Wataalam waonya dhidi ya kufunguliwa kwa shule kabla ya kufanikisha mikakati ya kuzuia maambukizi ya Covid-19

Wanafunzi
Wanafunzi
Washika dau katika sekta ya elimu wamemtaka waziri wa elimu George Magoha kuwa mwangalifu anapopanga mikakati ya kufunguliwa kwa shule ambazo zilifungwa kutokana na janga la Covid-19.

Magoha siku ya Jumatatu alidokeza kuwa huenda shule zikafunguliwa mapema kuliko ilivyotarajiwa mwezi Januari mwakani baada ya takwimu za wizara ya afya kuonyesha kwamba maambukizi ya virusi vya Corona yamepungua nchini.

Ukweli hata hivyo ni kwamba miezi sita tangu kufungwa kwa shule hizo mwezi Machi, hakuna mikakati ya kuimarisha usalama wa wanafunzi iliyowekwa ili kufanikisha mipango ya kufunguliwa kwa shule.

Ni kutokana na sababu hii ambapo mwenyekiti wa muungano wa walimu wakuu wa shule za upili Indimuli kahi alisema taasisi nyingi za elimu haziko tayari kwa ufunguzi huo.

"Changamoto nyingi ni katika shule za umma ambazo kwa kawaida huwa hata haziwezi kutekeleza kanuni za umbali ya futi sita kutokana na idadi kubwa ya wanafunzi," Kahi alisema.

Kufikia sasa shule bado hazina muongozo kuhusu cha kufanya wala fedha za kutekeleza mabadiliko ili kuafikia kanuni zilizowekwa na wizara ya afya.

"Ukweli ni kwamba shule bado ziko tu vile zilikuwa mwezi Machi na walimu wakuu hawajui la kufanya," Mwalimu wa shule ya upili aliambia.

Muungano wa walimu wakuu wa shule za msingi pia unasema hakuna hatua zilizochukuliwa kuweka mikakati tayari kukaribisha wanafunzi shule zitakapofunguliwa.

Siku ya Jumatatu, mkuu wa kitengo cha maradhi ambukizi katika hospitali kuu ya Kenyatta Loice Ombajo alionya kwamba kufungunguliwa kwa shule kabla ya kuwekwa kwa mikakati mahsusi ya kuzuia maambukizi huenda kukahujumu juhudi za serikali kukabili maambukizi ya virusi vya corona.