Orengo amtaka Ruto kumweleza Uhuru tofauti zake na Matiang'i

Muhtasari

• Orengo anasema ana habari kuwa Ruto alizomewa sana katika mkutano wa baraza la mawaziri siku ya Alhamisi.

• Ripoti zimeibuka kwamba mkutano huo ulikuwa moto wakati baraza hilo likijadili hatua kali za kudhibiti jolo la kisiasa ambalo limeanza kushika kasi nchini.

• Orengo aliwakumbusha wakenya kuhusu sheria kali za usalama zilizolazimishwa bungeni na Jubilee.

 

Seneta wa Siaya James Orengo amemtaka Naibu Rais William Ruto kuwasilisha tofauti zake na waziri wa usalama wa ndani Fred Matiang’i kwa rais Uhuru Kenyatta.

Orengo, ambaye ni mwandani wa Kinara wa ODM Raila Odinga alisema kwamba Ruto pia anafaa kuwasilisha tofauti zao kwa baraza la mawaziri.

Orengo anasema ana habari kuwa Ruto alizomewa sana katika mkutano wa baraza la mawaziri siku ya Alhamisi.

 

Ripoti zimeibuka kwamba mkutano huo ulikuwa moto wakati baraza hilo likijadili hatua kali za kudhibiti jolo la kisiasa ambalo limeanza kushika kasi nchini.

“Nataka kumwambia Ruto kwamba ikiwa ana tofauti zozote na Matiang’i aziwasilishe kwa baraza la mawaziri. Wakati wa mkutano wa mawaziri siku ya Alhamisi watu walianza kuuliza masuali na Ruto hangeweza kuyajibu,” Orengo alisema.

Orengo aliwakumbusha wakenya kuhusu sheria kali za usalama zilizolazimishwa bungeni na Jubilee.

Alisema kwamba sheria hizo ambazo Ruto na wandani wake waliunga mkono zimerejea kuwa kuwahangaisha.

“Ikiwa ataona teargas anafaa kujua kwamba ni sheria ambayo yeye alipitisha,” Orengo alisema.

Muungano wa NASA ulipinga vikali sheria hiyo na hata kuelekea mahakamani kutaka itupiliwe mbali.

Ni vipengele vichache vya sheria hiyo vilivopatikana kukiuka katiba.

 

Wafuasi wa naibu rais William Ruto walirushiwa vitoa machozi siku ya Alhamisi mjini Kisii na mkutano wake kutawanywa na maafisa wa usalama.