Uhuru Kenyatta atuma risala za rambirambi kwa familia ya Malombe

Muhtasari
  • Rais Uhuru Kenyatta ameifariji familia ya aliyekuwa Gavana wa Kitui Julius Malombe kufuatia kifo cha mkewe Edith Malombe

Rais Uhuru Kenyatta ameifariji familia ya aliyekuwa Gavana wa Kitui Julius Malombe kufuatia kifo cha mkewe Edith Malombe.

Katika ujumbe wake wa kufariji, mkuu wa nchi aliomboleza Mama Edith kama mwanasheria mashuhuri na gwiji wa haki za kijamii ambaye kifo chake kilikuwa pigo kubwa kwa nchi.

"Kifo cha Mama Edith sio tu pigo kubwa kwa familia ya rafiki yangu Dkt Julius Malombe bali pia kwa maelfu ya Wakenya ambao walinufaika moja kwa moja au kwa njia isiyo ya moja kwa moja kutokana na ustadi wake kama wakili na mpigania haki za kijamii," Uhuru alisema kwenye taarifa yake. Jumatano.

Alimtaja aliyekuwa mke wa gavana wa zamani wa kaunti ya Kitui kama mwanamke mwema mwenye imani ya kina na aliyejivunia kuwa kiongozi mwerevu na anayetegemewa.

"Katika maisha yake yote ya umma, Mama Edith aliendelea kuunda fursa kwa wengine kustawi," Uhuru alisema.

Mama Edith alihudumu kama Mama wa Kwanza wa Kitui kati ya Machi, 2013 na Agosti, 2017.

Uhuru alizidi kumpongeza kama mchangiaji katika huduma ya afya ya Kenya kwa kufanya kazi kwa karibu na mpango wa Bibi wa Rais Margaret Kenyatta wa Beyond Zero kupanua ufikiaji wa huduma ya afya ya uzazi katika kaunti hiyo.

"Kama nchi, tuna deni la kumshukuru Mama Edith kwa kazi aliyoifanya kwa miaka mingi kuifanya Kenya kuwa nchi bora kwa wote," Uhuru alisema.

Rais aliiombea Mungu faraja familia ya Julius Malombe na marafiki wakati wakiendelea kukubaliana na kifo cha Mama Edith.

Familia ya Malombe ilitangaza kifo cha Mama Edith Jumatano asubuhi.