Mlinzi aliyedaiwa kupigwa risasi na Didmus Barasa hatimaye azikwa Kakamega

Aliyekuwa mwajiri wa marehemu, mgombea ubunge Brian Khaemba aliomba muuaji wake asiwahi kupata amani.

Muhtasari

•Olunga ambaye alikuwa na umri wa miaka 21 tu alipokumbana na mauti yake alizikwa Jumamosi katika hafla iliyojaa huzuni na majonzi mengi.

•Mgombea ugavana Fernandes Barasa alitoa wito kwa mamlaka kuhakikisha kuwa mhusika amepata adhabu inayomfaa.

Image: FACEBOOK// WAKILI BRIAN KHAEMBA

Marehemu Brian Odinga Olunga, dereva wa mgombea ubunge wa Kimilili jkwa tiketi ya DAP-K Brian Khaemba aliyedaiwa kuuawa na mbunge Didmus Barasa  hatimaye alizikwa nyumbani kwao Samiti,eneo bunge la Navakholo, Kaunti ya Kakamega.

Olunga ambaye alikuwa na umri wa miaka 21 tu alipokumbana na mauti yake alizikwa Jumamosi katika hafla iliyojaa huzuni na majonzi mengi.

Mamia ya wenyeji, vijana na wanasiasa kadhaa walihudhuria mazishi ya mwanafunzi huyo wa Chuo Kikuu cha Masinde Muliro.

Huku akimuomboleza, aliyekuwa mwajiri wa Olunga, Brian Khaemba ambaye alipoteza kinyang'anyiro cha ubunge kwa Barasa katika uchaguzi wa Agosti 9 aliomba muuaji asiwahi kupata amani.

""Nenda sawa kaka yangu, namesake wangu na  mlinzi wangu Brian Olunga. Muuaji wako asijue amani ulimwenguni huu na katika ulimwengu ujao. Mpaka tukutane tena kwenye ufuo huo mzuri," Khaemba alisema.

Mgombea ugavana wa Kakamega kwa tiketi ya ODM Fernandes Barasa alitoa wito kwa mamlaka kufanya uchunguzi wa kina kuhusiana na mauaji na Olunga na kuhakikisha kuwa mhusika amepata adhabu inayomfaa.

"Ilikuwa wakati wa hisia sana huko Samitsi, Kaunti Ndogo ya Malava tulipokuwa tukimzika Brian Olunga. Marehemu aliuawa tarehe 9 Agosti huko Kimilili. Natoa wito kwa mamlaka kuharakisha uchunguzi wa mauaji haya ya kipumbavu ili wahusika waweze kuchukuliwa hatua," Barasa alisema kwenye Twitter.

Marehemu alizikwa huku Barasa ambaye anadaiwa kutekeleza mauaji yake akiendelea kuzuiliwa katika kituo cha polisi cha Bungoma.

Barasa alijisalimisha mikononi mwa polisi mnamo Agosti 12 baada ya msako dhidi yake kutangazwa.

Mnamo Jumanne mahakama iliamuru mshukiwa asalie rumande kwa siku 10 zaidi ili kuwapatia wapelelezi muda wa kukamilisha na kuwasilisha ripoti za uchunguzi na mwili na wa silaha iliyotumika katika mauaji.

Kesi hiyo itatajwa tena mnamo Agosti 24 kwa DPP kuthibitisha hali ya upelelezi kabla ya kutoa uamuzi wa kushtakiwa.