Uhuru anafadhili maandamano ya Azimio ya kuvuruga utawala wa Ruto - Ichung'wa

Ichung'wa anadai Uhuru bado anapata ugumu kukubali ushindi wa Kenya Kwanza.

Muhtasari

•Ichung’wa amedai kuwa Rais wa zamani Uhuru Kenyatta ndiye mfadhili mkuu wa maandamano yaliyopangwa za Azimio la Umoja.

•Ichungwa alizidi kumkashifu Uhuru akisema anastahili kulaumiwa kwa ‘uasi’ wa kiongozi wa ODM Raila Odinga.

akizungumza katika Kianyaga Boys Jumamosi.
Kiongozi wa walio wengi katika Bunge la Kitaifa Kimani Ichung'wa akizungumza katika Kianyaga Boys Jumamosi.

Kiongozi wa Wengi katika Bunge la Kitaifa Kimani Ichung’wa amedai kuwa Rais wa zamani Uhuru Kenyatta ndiye mfadhili mkuu wa maandamano yaliyopangwa za Azimio la Umoja.

Jumamosi, Ichung’wa alidai kuwa Uhuru akiwa nyuma ya pazia anafadhili maandamamo hayo yaliyoratibiwa na kinara wa ODM Raila Odinga.

Akizungumza katika Shule ya Upili ya Wavulana ya Kianyaga katika kaunti ya Kirinyaga, wakati wa mkutano wa wanafunzi wa zamani, Ichung’wa alisema maandamano hayo ni sehemu ya mpango mkubwa zaidi wa Rais wa zamani wa kuuvuruga utawala uliopo.

Anadai Uhuru bado hajakubali na anapata ugumu kuamini ushindi wa Kenya Kwanza.

"Ni wakati muafaka wa kukubali kwamba Ruto ambaye wakati mmoja alikuwa naibu wako na Rigathi ambaye wakati mmoja alikuwa msaidizi wako wa kibinafsi sasa ni Rais na Naibu Rais wa Kenya mtawalia," Ichung'wa alisema.

"Ikiwa bado unafikiri wao ni wadogo wako bora ukubali ukweli, na mapema ufanyapo, ni bora zaidi. Huwezi kufanya lolote kuwazuia kutawala nchi."

Raila amekanusha madai hayo akisema maandamano ya umma yanafadhiliwa na wananchi wenyewe.

Katika mahojiano na vyombo vya habari siku ya Jumamosi, Raila alisema maandamano ya umma yanafadhiliwa kikamilifu na wananchi.

"Maandamano haya hayajafadhiliwa na mtu mmoja maalum. Yanafadhiliwa na wananchi wenyewe. Hakuna mtu mwenye kiasi kikubwa cha fedha cha kumudu gharama za harakati." alisema.

Ichungwa alizidi kumkashifu Uhuru akisema anastahili kulaumiwa kwa ‘uasi’ wa kiongozi wa ODM Raila Odinga.

“Kupitia uzembe wako wa kisiasa na kwa nia moja pekee ya kumzuia naibu wako asipande urais ulimfufua mwana kitendawili licha ya sisi kumshinda katika uchaguzi wa 2017. Wewe si Mungu na tulikuambia kwamba hatutakuabudu lakini tutakuheshimu,” alisema.

Ichung’wa alisema kuwa ni tendo la kutowajibika kwa Azimio kuwachochea Wakenya kuhusu gharama ya juu ya maisha ilhali wao wana mchango katika msukosuko wa kiuchumi uliopo nchini.

“Nani alichukua gharama ya maisha hapa ilipo leo ikiwa sio utawala wa handshake chini ya Uhuru Kenyatta na Raila Odinga? Acheni kuwachokoza Wakenya na muwaruhusu Ruto na Rigathi kurekebisha uchumi mliofanya fujo kwa sababu wana mpango wazi wa jinsi ya kufufua uchumi mliouacha kwenye shimo refu,” akasema.