Sakaja atishia kuwatimua madaktari wanaogoma Nairobi

Muhtasari
  • Gavana alihimiza Muungano wa KMPDU tawi la Nairobi kutafuta mbinu mbadala za kueleza matakwa yao bila kuvuruga huduma za afya jijini Nairobi.
Gavana Sakaja ndani ya studio za Radio Jambo
Image: BRIAN SIMIYU

Gavana wa Nairobi Johnson Sakaja amewataka madaktari wa kaunti ya Nairobi wanaogoma kurejea kazini mara moja.

Akihutubia wanahabari Jumatano jioni, Gavana Sakaja aliwapa madaktari jijini Nairobi saa 12 kurejea kazini, akisisitiza kuwa hataruhusu maisha ya wagonjwa kusalia hatarini kwa masuala anayosema yanaweza kutatuliwa hatua kwa hatua.

Gavana huyo wa Nairobi aliongeza kuwa masuala ya serikali ya kitaifa kushindwa kuwapa wanafunzi wanaosomea udaktari na kutoheshimu Mkataba wa Makubaliano (CBA)  2017 hayahusiani moja kwa moja na mamlaka ya kaunti hivyo basi madaktari walioajiriwa na kaunti ya Nairobi wanapaswa kurejea kazini. 

“Nimewapa madaktari wa Nairobi saa 12 kujitokeza katika hospitali zetu. Wale wanaotaka kuendelea kufanya kazi katika kaunti ya Nairobi mna saa 12 za kujitokeza katika hospitali zetu kwa sababu jukumu nililonalo ni kuhakikisha kuwa ninatoa huduma za afya kwa wakazi wa Nairobi,” alisema Sakaja.

Gavana alihimiza Muungano wa Madaktari, Wafamasia na Madaktari wa Meno nchini (KMPDU) tawi la Nairobi kutafuta mbinu mbadala za kueleza mshikamano na maswala ya tawi la kitaifa bila kuathiri huduma ya wagonjwa jijini Nairobi.

"Ninataka kuwasihi KMPDU, tawi la Nairobi kwamba kuna njia tofauti za kuonyesha mshikamano na tawi la kitaifa ambalo lina maswala na serikali ya kitaifa bila kuhatarisha au kuweka sawa maisha ya Nairobi, ambayo serikali yake huna maswala yoyote ya kuenda mgomo,” alisema

Gavana huyo alibainisha kuwa madaktari ambao watakuwa hawajaripoti kazini kufikia Alhamisi asubuhi watachukuliwa kuwa hawana nia ya kufanya kazi na Kaunti ya Nairobi, akiongeza kuwa utawala wake utatekeleza wajibu wake wa kikatiba kujaza nyadhifa hizo.

Alisisitiza kuwa ingawa anaheshimu haki za madaktari kueleza malalamishi yao, kugoma kuhusu masuala na mwajiri tofauti si halali wanaposambaratisha huduma za afya za wakazi wa Nairobi.

Muungano wa KMPDU na serikali kufikia sasa wamefanya mikutano miwili ili kuondoa mkwamo uliopo, lakini hakuna uliotoa matokeo yaliyotarajiwa.

Pande zote mbili zitakutana kwenye meza ya mazungumzo tena Alhamisi kwa mkutano utakaoitishwa na Mkuu wa Utumishi wa Umma na kutekelezwa na mahakama.