Madaktari kuanza kutekeleza mgomo kuanzia saa sita usiku hii leo

Katibu Mkuu wa KMPDU Davji Atellah alilaumu serikali kwa kusitasita kutafuta suluhu, licha ya kuwepo kwa mazungumzo.

Muhtasari

• Atellah almeema kuwa licha ya notisi yao ya mgomo wa siku saba za awali, serikali imekataa kushughulikia masaibu ya wafanyikazi wa afya.

akiwahutubia wanahabari tarehe 17 Novemba 2023.
Katibu Mkuu wa KMPDU Dkt. Davji Atellah akiwahutubia wanahabari tarehe 17 Novemba 2023.
Image: HISANI

Muungano wa Madaktari na Madaktari wa Meno nchini Kenya umetoa notisi ya mgomo wa kitaifa kuanzia leo saa sita usiku.

Katibu Mkuu wa KMPDU Davji Atellah, katika taarifa yake amesema uamuzi huo uliafikiwa kutokana na kutokuwepo kwa maelewano na serikali kuhusu masuala yanayowahusu wahudumu wa afya kote nchini.

Atellah almeema kuwa licha ya notisi yao ya mgomo wa siku saba za awali, serikali imekataa kushughulikia masaibu ya wafanyikazi wa afya.

"Kwa kusikitisha, serikali imeonyesha ukosefu wa utayari wa kushughulikia maswala haya makubwa, na kuwaacha wafanyikazi wa afya katika hali ya kufadhaika .

Kwa hiyo, kwa masikitiko makubwa tunatangaza kuanza kwa mgomo wa nchi nzima kuanzia saa sita usiku leo ​​Machi 13, 2024,” alisema Sec-Gen.

Mkuu huyo wa KMPDU alilaumu serikali kwa kusitasita kutafuta suluhu, licha ya kuwepo kwa mazungumzo.

“Ndani ya siku saba za notisi ya mgomo, muungano umeonyesha nia ya kushiriki katika Mazungumzo. Hata hivyo, tulichoshuhudia ni ukosefu wa umakini kutoka kwa serikali pamoja na kutokuwepo kwa nia njema,” aliongeza.

Awali madaktari walikuwa wametishia kushiriki katika mgomo iwapo mahitaji yao Mkataba wa Mapatano ya Pamoja wa 2017 (CBA) hautatekelezwa.

Muungano huo pia ulikuwa umetaka kurejeshewa ushuru wa nyumba uliokatwa, ukitaja kuwa ni kinyume cha sheria.