Bashasha huku mahasidi Diamond na Harmonize wakikutana na kufurahia pamoja

Mshindani mwingine wa Diamond, Alikiba pia alikuwepo katika ikulu wakati wa hafla hiyo

Muhtasari

•Diamond na Harmonize, mnamo Jumanne jioni walipata fursa adimu ya kuwa kwenye ukumbi mmoja baada ya muda mrefu sana.

•Wawili hao waliokuwa wamevalia mavazi yanayoenda kufanana walionekana kufurahi sana kukutana na wakafanya mazungumzo yasiyosikika.

Diamond na Harmonize
Image: INSTAGRAM// MWIJAKU

Mastaa wawili wa bongofleva, Diamond Platnumz na Harmonize, mnamo Jumanne jioni walipata fursa adimu ya kuwa kwenye ukumbi mmoja baada ya muda mrefu sana.

Wawili hao wanaoaminika kuwa wapinzani wakubwa katika tasnia ya muziki wa bongo fleva walikutana na hata kusalimiana katika Ikulu ya Tanzania wakati wa sherehe za Iftar iliyoandaliwa na rais Samia Suluhu Hassan.

Mburudishaji Mwijaku alishiriki picha na video za mkutano wao mzuri, na akajipiga kifua kuwa aliwafanya wakutane.

"Nguvu ya mama imeonekana leo, Samia Suluhu Hassan!! Leo nimewakutanisha Diamond Platnumz na Harmonize, nikasema hakuna ninachoweza kushinda!!," Mwijaku alijigamba.

Katika moja ya video alizoshiriki mburudishaji huyo, Harmonize alionekana akimsalimia aliyekuwa bosi wake Diamond ambaye alikuwa amekaa chini.

Wawili hao ambao walikuwa wamevalia kanzu nzuri zinazoenda kufanana walionekana kufurahi sana kukutana na wakafanya mazungumzo yasiyosikika.

“Nguvu ya Mama haina mpinzani, Samia Suluhu Hassan amenipa maagizo na nimeyatekeleza! Watu muhimu sana! Diamond Platnumz na Harmonize tayari wameshapeana mikono hapa Ikulu,” aliandika Mwijaku chini ya video hiyo.

Pia alishiriki picha zaidi za mastaa hao wawili wakubwa wa bongo pamoja na watu wengine mashuhuri kwenye ikulu ya serikali.

Mshindani mwingine wa Diamond, Alikiba pia alikuwepo katika ikulu wakati wa hafla hiyo lakini haijafahamika iwapo wao pia walipata kukutana na kuzungumza

Jux, Maua Sama na mchekeshaji Joti ni miongoni mwa mastaa wengine waliohudhuria sherehe hizo.

Mashabiki wameendelea kusherehekea na kupongeza mkutano baina ya Diamond na Harmonize na kuwasihi wamalize uhasama na kudumisha uhusiano mzuri.