Diamond ashiriki mazugumzo mazito na Rick Ross, aahidi kumtafutia mke wa Kitanzania

Rick Ross aliahidi kutembelea Tanzania hivi karibuni ambapo ataburudika na Diamond na kufanya naye kazi

Muhtasari

•Walijadili mada nyingi zikiwemo muziki, kumbukumbu nzuri, albamu ijayo ya Diamond, ziara ya Rick Ross barani Afrika, utajiri na mali zao.

•Rick Ross aliahidi kumjumuisha Diamond katika mradi wake ujao wa Kiafrika na kutembelea bara hivi karibuni ili kufanya kolabo na wasanii chipukizi.

walishiriki mazungumzo mazito.
Diamond na Rick Ross walishiriki mazungumzo mazito.
Image: INSTAGRAM

Siku ya Jumapili jioni, staa wa Bongo, Naseeb Abdul Juma almaarufu Diamond Platnumz alishiriki gumzo la moja kwa moja kwenye Instagram na rapa mkongwe wa Marekani Rick Ross.

Waimbaji hao wawili walikuwa na mazungumzo marefu ambapo walijadili mada nyingi zikiwemo muziki, kumbukumbu nzuri, albamu ijayo ya Diamond, ziara ya Rick Ross barani Afrika, utajiri na mali zao.

Katika mazungumzo hayo, bosi huyo wa WCB alimsifu Rick Ross kwa kuunga mkono muziki wa Afrika kwa miaka mingi na kuwasapoti wasanii wa Afrika.

“Nataka nikupe sifa ya kipekee kwa sababu unakumbuka katika siku za nyuma hata P-Square walipokuwa wanafanya muziki, wewe ndiye uliyefanya nao wimbo. Kabla ya wasanii wengine wote wakubwa,” Diamond alimwambia Rick Ross katika mazungumzo hayo.

Aliongeza, “Hapo zamani ilikuwa ngumu, unajua baadhi ya wasanii hawakuwahi kuuchukulia muziki wa Kiafrika kwa uzito. Lakini ulianza kuchukua muziki wa Kiafrika kwa uzito tangu kitambo. Miaka mingi iliyopita. Unachukulia muziki wa Kiafrika kwa uzito, haijalishi unatoka wapi. Umesapoti na tunashukuru kwamba, unafungua njia kwa kizazi kijacho.”

Rapa huyo wa Marekani kwa upande wake aliahidi kumjumuisha Diamond katika mradi wake ujao wa Kiafrika na kutembelea bara hivi karibuni ili kufanya kolabo na wasanii chipukizi.

Pia aligusia kutaka kuburudika na staa huyo wa bongo fleva nchini Tanzania katika ziara yake ijayo ambayo alisema inakuja hivi karibuni.

"Nataka kuja huko na nataka kushirikiana na vijana. Sio hivyo tu, wacha tuburudike kifahari, ikiwa tutaenda kwenye kilabu katika jiji lako. Nataka unipeleke kwenye kilabu, tunataka kuruka, tunataka kuvaa, tuvae mapambo yetu, " alisema.

Diamond aliahidi kumpeleka rapa huyo katika klabu mpya inayomilikiwa na meneja wake Sallam SK na pia kumtafutia mke wa Kitanzania katika ziara hiyo.

"Na utakapokuja hapa, nitahakikisha nitakutafuta mke wa Kitanzania," alisema.

Rick Ross alionekana kukwepa pendekezo la Diamond la kumtafutia mke na kusema, “Utanipeleka kuzunguka jiji laki. Wacha tufanye hivi vikubwa.”

Staa huyo wa bongo fleva pia alichukua muda kumuonyesha Rick Ross utajiri wake na mkusanyiko wa magari yake mengi ya kifahari watakayotumia wakati wa ziara yake.