Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Mawasiliano Kenya (CA) Ezra Chiloba ajiuzulu

Chiloba alihudumu tangu 2021, baada ya kuchukua nafasi ya Francis Wangusi baada ya kustaafu

Muhtasari

•Mnamo Septemba, Chiloba alisimamishwa kazi kufuatia ukaguzi wa ndani uliomshutumu kwa ubadhirifu wa kifedha Hata hivyo alikanusha tuhuma hizo.

Ezra Chiloba
Image: Ezra Chiloba/TWITTER

Ezra Chiloba amejiuzulu wadhifa wake wa Meneja mkurugenzi wa Mamlaka ya mawasiliano nchini Kenya (CA) .

Chiloba alijiuzulu Jumatano katika barua iliyotumwa kwa mwenyekiti wa bodi ya wakurugenzi ya CA Mary Mungai.

Katika notisi, mnamo Alhamisi, Mungai alimshukuru Chiloba kwa mchango wake wa kipekee kwa mamlaka  hiyo.

"Kwa niaba ya mamlaka ninamtakia mkurugenzi mkuu anayemaliza muda wake mafanikio katika juhudi zake za baadaye na kuthamini mchango wake mkubwa kwa shirika na sekta pana ya ICT," alisema.

Chiloba alihudumu tangu 2021, baada ya kuchukua nafasi ya Francis Wangusi baada ya kustaafu.

Mnamo Septemba, Chiloba alisimamishwa kazi kufuatia ukaguzi wa ndani uliomshutumu kwa ubadhirifu wa kifedha hata hivyo alikanusha tuhuma hizo.

Kulingana na ukaguzi huo, Chiloba na maafisa wengine tisa wakuu katika mamlaka hiyo wanadaiwa kushughulikia vibaya mikopo ya nyumba na marupurupu ya kima cha mamilioni ya pesa.

Mkutano wa Kamati Maalum ya Ukaguzi  wa Bodi  uliofanyika Agosti 8 ulieleza kwa kina madai ya utovu wa nidhamu dhidi ya Chiloba.

Kulingana na ripoti hiyo, Chiloba na timu yake ya usimamizi katika mamlaka hiyo walisimamia ufadhili wa rehani ya hadi Sh364.8 milioni,ambacho ni kinyume cha sheria.

Katika ripoti hiyo Chiloba alidaiwa kutumia afisi yake kuidhinisha rehani yake, ikiashiria matumizi mabaya ya mamlaka, ambayo bodi inasema ni kosa chini ya kifungu cha 41 na 42 cha Mapambano ya Kupambana na Ufisadi.

Inadaiwa kuwa Chiloba aliomba na kujiidhinishia mkopo wa rehani ili kuwezesha ununuzi wa mali kati yake na Jacob Simiyu Wakhungu, bila kuwasilisha maelezo ya shughuli hiyo kupigwa msasa na kuidhinishwa na mamlaka ya juu.

Ripoti hiyo ilisema kwamba alinunua nyumba na kipande cha ardhi cha ekari saba, idadi iliyozidi kiwango kinachohitajika cha ekari moja kinyume na matakwa ya mpango wa makazi ya watumishi wa umma.