Polisi wamsaka mganga aliyemdunga mwanamke mjamzito msumari kichwani

Muhtasari

•Mwanamke huyo alifika katika hospitali ya Peshawar baada ya kujaribu kuchomoa msumari wa 5cm (inchi mbili) kwa koleo.

Picha ya X ray inaonyesha msumari uliokwama kwenye kichwa cha mwanamke
Picha ya X ray inaonyesha msumari uliokwama kwenye kichwa cha mwanamke
Image: LADY READING HOSPITAL

Msako unaendelea nchini Pakistani kumtafuta mganga mmoja anayedaiwa kushindilia msumari kwenye kichwa cha mwanamke mjamzito.

Mwanamke huyo alifika katika hospitali ya Peshawar baada ya kujaribu kuchomoa msumari wa 5cm (inchi mbili) kwa koleo.

Awali, aliwaambia madaktari kuwa alitekeleza kitendo hicho yeye mwenyewe, lakini baadaye alikiri mganga mmoja ambaye alidai kuwa anaweza kumhakikishia kujifungua mtoto wa kiume alihusika.

Polisi walianza kuchunguza baada ya picha za x-ray za jeraha kuonekana mtandaoni.

Dk Haider Khan, mfanyakazi katika Hospitali ya Lady Reading, alisema mwanamke huyo "alikuwa na fahamu kabisa, lakini alikuwa katika maumivu makali," alipofika kutafuta matibabu.

Wafanyikazi katika hospitali hiyo waliambia gazeti la Dawn kwamba mwanamke huyo alimwendea mganga huyo baada ya kusikia kuhusu mila hiyo kutoka kwa jira

Waliongeza kuwa mwanamke huyo alikuwa mama wa watoto watatu wa kike, na kwamba mumewe alikuwa ametishia kumwacha iwapo angejifungua mtoto mwingine wa kike.

"Ana ujauzito wa miezi mitatu na kwa sababu ya hofu ya mumewe alienda kwa mganga wa kienyeji" wahudumu wa hospitali waliambia Dawn.

Katika baadhi ya nchi maskini zaidi kusini mwa bara Asia, mtoto wa kiume mara nyingi anaaminika kutoa usalama bora wa kifedha wa muda mrefu kwa wazazi kuliko watoto wa kike, na hii inasababisha vitendo vya unyonyaji, mara nyingi kwa wale wanaoitwa "waganga wa imani".

Waponyaji imani ni watu wa kawaida katika baadhi ya maeneo ya Pakistani, hasa katika maeneo ya kaskazini-magharibi. Matendo yao yanatokana na ngano za Kisuf.

Shughuli zao zimepigwa marufuku hata katika shule nyingi za Kiislamu.

Katika ujumbe wa Twitter uliotolewa siku ya Jumanne, mkuu wa polisi wa Peshawar, Abbas Ahsan alisema kwamba timu maalum ya uchunguzi imeundwa ili "kumfikisha mahakamani yule aliyecheza na maisha ya mwanamke asiye na hatia na kumtia msumari kichwani.

Polisi wametumia siku kadhaa wakiwahoji wahudumu wa hospitali hiyo na kujaribu kumsaka mwanamke huyo ambaye alitoka hospitali baada ya wahudumu kumng'oa msumari huo kichwani kwa matumaini kwamba anaweza kuwasaidia kumtambua mwanaume huyo.

"Hivi karibuni tutamtia mbaroni mganga huyo," Bw Ahsan alisema.

Bw Ahsan pia alisema kuwa maafisa wake watachunguza ni kwa nini wafanyikazi hao walikosa kuripoti tukio hilo kwa polisi mwanamke huyo alipowasili hospitalini kwa mara ya kwanza.