Mama alilia haki baada ya mwanawe kupigwa hadi kufa na mlinzi katika shule ya Embu

Muhtasari

•Dennis Macharia ambaye alikuwa mwanafunzi katika shule ya ufundi ya Karurumo anadaiwa kupigwa na mlinzi wa kituo hicho kwa madai ya wizi wa nyaya za umeme na vyuma.

•Deborah Muthoni ambaye ni mamake Macharia, alisema hakuamini alipoambiwa kuhusu kilichompata mwanawe.

•Shule hiyo ilifungwa  mara moja siku ya Jumanne kwa kipindi kisichojulikana hadi taarifa zaidi itakapotolewa kufuatia tukio hilo.

Deborah Muthoni, mamake Macharia akiongea na wanahabari katika eneo la Karurumo mnamo Februari 8
Deborah Muthoni, mamake Macharia akiongea na wanahabari katika eneo la Karurumo mnamo Februari 8
Image: BENJAMIN NYAGAH

Polisi katika kaunti ya Embu wanachunguza kisa kimoja ambapo mwanafunzi mwenye umri wa miaka 20 anaripotiwa kupigwa na mlinzi vibaya hadi ni kifo.

Dennis Macharia ambaye alikuwa anasomea kozi ya uwekaji wa umeme katika shule ya ufundi ya Karurumo anadaiwa kupigwa na mlinzi wa kituo hicho kwa madai ya wizi wa nyaya za umeme na vyuma.

Akithibitisha tukio hilo naibu kamishna wa kaunti ndogo ya Embu Mashariki George Omollo alisema kwamba polisi walipokea ripoti kuhusu tukio  hilo mwendo wa saa nne unusu asubuhi ya Jumatatu kisha wakakimbia mpaka eneo la tukio ambapo walipata mwanafunzi huyo akiwa amejeruhiwa vibaya.

Macharia alipofikishwa katika kituo cha afya cha Karurumo alithibitishwa kufariki na mwili wake kupelekwa katika hifadhi ya maiti ya hospitali ya Ena Tenri.

Omollo alisema kuwa mtu mmoja anazuiliwa  na polisi ili kusaidia katika uchunguzi. Aliwahakikishia wakazi kuwa yeyote atakayepatikana na hatia atakabiliwa na sheria.

Kulingana na mwanafunzi aliyeshuhudia tukio hilo, mnamo Jumatatu asubuhi mlinzi huyo aliwashambulia kinyama wavulana watatu ambao aliwashtumu kwa wizi.

Joseph Kinyua (sio jina lake halisi) alisema mlinzi huyo aliwachapa wavulana hao watatu kwa kutumia mijeredi lakini alikuwa mkali zaidi kwa Macharia.

Kinyua alisema walimu kadhaa walijaribu kumsihi mlinzi huyo aache lakini akatia masikio yake pamba  na kuendelea.

Wavulana hao walipopelekwa katika afisini ya shule ili kuhojiwa, Macharia alianguka chini na kuwalazimu wasimamizi wa shule kumkimbiza katika kituo cha afya cha Karurumo.

"Kama mwanafunzi ninahisi siko salama kwani sheria hapa inatumika kikatili," alisema Kinyua.

Deborah Muthoni ambaye ni mamake Macharia, alisema hakuamini alipoambiwa kuhusu kilichompata mwanawe.

Karurumo Vocational Training Centre
Karurumo Vocational Training Centre
Image: BENJAMIN NYAGAH

Aliwataka polisi kuhakikisha haki inatendeka na mhusika anakamatwa na kufunguliwa mashtaka.

“Naviomba vyombo husika vifanye uchunguzi wa kina na kuhakikisha aliyehusika na kifo cha mwanangu anakamatwa na kufikishwa mahakamani,” alisema.

Muthoni alisema kuwa iwapo madai ya wizi yalikuwa ya kweli mwanawe alipaswa kukamatwa badala ya kuadhibiwa vikali.

Alisema kuwa Macharia alikuwa tumaini la familia yake kwani alikuwa na mchango mkubwa katika maisha ya nduguye watatu.

Shule hiyo ilifungwa  mara moja siku ya Jumanne kwa kipindi kisichojulikana hadi taarifa zaidi itakapotolewa kufuatia tukio hilo.

Meneja wa shule hiyo Dolly Mutembei alidinda kuzungumzia kilichotokea na badala yake akasema ameacha suala hilo kwa mamlaka.

Hata hivyo alisema kuwa usimamizi wa shule unapanga mkutano na wazazi wa Macharia. 

"Kwa sasa tunapanga kukutana na wazazi. Ofisi ya DCI inahusika na inashughulikia kesi hiyo na ndiyo maana siwezi kusema mengi kuihusu," alisema Mutembei.