Mwanadada afungwa gerezani miaka 14 kwa kumnyonga mumewe hadi kifo

Muhtasari

•Maureen Chebet alihukumiwa baada ya kukubali mashtaka ya kuua aliyekuwa bwanake Elias Kipchirchir Yego bila kukusudia.

•Mnamo siku ya tukio, wapenzi hao wawili walizozana kabla ya mshtakiwa kumnyonga marehemu hadi kifo.

Mahakama
Mahakama

Mwanamke anayetuhumiwa kunyonga bwanake hadi kifo miaka minne iliyopita amehukumiwa kifungo cha miaka 14 gerezani.

Maureen Chebet alihukumiwa baada ya kukubali mashtaka ya kuua bwanake Elias Kipchirchir Yego bila kukusudia mnamo Februari 17, 2018 katika eneo la Kapsabet, kaunti ya Nandi.

Katika hukumu iliyotolewa na hakimu Reuben Nyakundi mnamo Februari 3, mahakama ilizingatia kukiri hatia kwa mshtakiwa, na kumhukumu kifungo cha miaka 15.

Mahakama hata hivyo  ilibaini kuwa mshtakiwa alikuwa kizuizini kuanzia Machi 8, 2018 hadi sasa na kwa hivyo kuzingatia kupunguza kifungo.

Hakimu Nyakundi hata hivyo alisema kuwa kosa la mshtakiwa lilikuwa kubwa na hakukuwa na sababu za kupunguza kifungo kwa hivyo akakata mwaka mmoja tu kutoka kwa hukumu ya hapo awali.

Alisema hakukuwa na sababu tosha za kupelekea upunguzaji wowote wa kifungo na kumhukumu miaka 14.

Chebet aliingia katika makubaliano ya mazungumzo mnamo Februari 2, 2020.

Mkataba wa makubaliano hayo ulipendekeza ashtakiwe kwa kuua bila kukusudia na kuhukumiwa kifungo cha miaka 10.

Mahakama ilisikia kwamba Chebet alikuwa akiishi pamoja na marehemu na ugomvi wao mara nyingi ulishuhudiwa na majirani.

Mnamo siku ya tukio, wapenzi hao wawili walizozana kabla ya mshtakiwa kumnyonga marehemu hadi kifo.

Akikubali makosa yake, Chebet alisema alijuta matendo yake na kueleza kuwa yeye ni mama wa watoto wanne, akiwemo mtoto mmoja aliyezaa pamoja na mwanamume ambaye aliua.

“Mahakama hii inaona kwamba mshtakiwa lazima awajibikie matendo yake kikamilifu. Mshtakiwa lazima ajifunze jinsi ya kudhibiti hisia zake ili kuepuka kuwadhuru wengine,” hakimu alisema.