Takribani watu 400 wapoteza maisha, 801 wajeruhiwa Ukraine - UN

Muhtasari
  • Kulingana na takwimu za hivi punde za Umoja wa Mataifa, watu 1,207 wamepata madhara tangu uvamizi wa Urusi nchini Ukraine kuanza tarehe 24 Februari
Image: Reuters

Kulingana na takwimu za hivi punde za Umoja wa Mataifa, watu 1,207 wamepata madhara tangu uvamizi wa Urusi nchini Ukraine kuanza tarehe 24 Februari.

Idadi hiyo inajumuisha watu 406 waliouawa na 801 kujeruhiwa - lakini takwimu "zina uwezekano mkubwa kuwa idadi zaidi ya hiyo" anasema Liz Throssell, msemaji wa Kamishna Mkuu wa Umoja wa Mataifa wa Haki za Kibinadamu.

Majeraha mengi ni matokeo ya "mashambulio ya anga na silaha za milipuko", unasema Umoja wa Mataifa, na "mamia ya majengo ya makazi" yameharibiwa katika miji kote Ukraine.

Mwanahabari mmoja anaripotiwa kuuawa. Umoja wa Mataifa pia umeelezea wasiwasi wake kuhusu "kukamatwa kiholela" kwa wafuasi wanaounga mkono Ukraine katika maeneo yaliyo chini ya udhibiti wa kijeshi wa Urusi - pamoja na ghasia dhidi ya wale wanaochukuliwa kuwa wanaounga mkono Urusi katika maeneo yanayodhibitiwa na serikali ya Ukraine.

Takwimu za hivi punde za Umoja wa Mataifa zinaonesha takriban watu 12,700 wamekamatwa nchini Urusi kwa kufanya maandamano ya amani ya kupinga vita.

Shirika hilo lilikosoa "sheria kandamizi" zilizowekwa na Urusi hivi karibuni ambazo zinaweka kifungo cha hadi miaka 15 jela kwa wale wanaoshtakiwa kwa kueneza habari iliyoitwa ya "uongo" kuhusu uvamizi huo, au kudharau vikosi vya jeshi la Urusi.