Mbunge asema bando zinazo'expire ni kuibia watu, ataka sheria hiyo kuharamishwa

Simu ni ya kwangu, nimenunua bando kwa fedha yangu, halafu unanilazimisha nitumie kwa muda unaotaka wewe - mbunge Mitinga aliuliza.

Muhtasari

• "Tunahitaji mswada wa kuhusu kulinda haki zetu. Mashirika haya ya mawasiliano yamekuwa yakituibia mheshimiwa spika" - mbunge Mitinga alisema.

Mbunge Francis Mitinga
Mbunge Francis Mitinga
Image: YouTube screengrab

Mbunge mmoja nchini Tanzania amezua mjadala mitandaoni baada ya kutilia shaka uhalali wa vifurushi vya deta za intaneti kufikia kikomo cha matumizi yake hata kama kifurushi hakijaisha.

Mbunge Francis Mitinga alikuwa akiwasilisha hoja bungeni huku akisema kuwa mashirika ya mawasiliano yanaibia watu pasi na wao kujua kwa kuweka muda na tarehe maalum kwa vifurushi vya deta ya mtandaoni yaani bando.

Akijadiliana na Bunge la nchi hiyo, Mtinga alitoa maoni kuwa kuweka tarehe ya mwisho ya matumizi ya data za simu na makampuni ya mawasiliano kuharamishwe.

“Mawasiliano ni muhimu katika uchumi wa nchi yetu. Tunahitaji mswada wa kuhusu kulinda haki zetu. Mashirika haya ya mawasiliano yamekuwa yakituibia mheshimiwa spika. Hivi ni kwa nini bando zina-expire? Simu ni ya kwangu, nimenunua bando kwa fedha yangu, halafu unanilazimisha nitumie kwa muda unaotaka wewe. Hii kwa nini? Kama ni sheria, iletwe hapa tuibadilishe,” mbunge Mitinga alisema.

Kulingana na mbunge huyo, sheria hiyo inafaa kuharamishwa kwa kile alisema ni wizi wa mchana peupe kwa jasho la wananchi wanaotafuta pesa zao na kununua simu kwa ajili ya mawasiliano lakini anawekewa mikakati ya kumalizika kwa bando hiyo chini ya siku saba.

“Tunaibiwa tukiona, kwa nini unipangie kutumia bando langu? Mimi si ndio najua umuhimu wa mawasiliano ndio maana nikanunua lile bando la wiki moja. Kama nimeamua kulitumia taratibu wiki moja imeisha nimeweka akiba, kwa nini wewe ulikate?” mbunge alisema huku wabunge wenzake wakimshangilia.

Je, maoni yako ni yepi kuhusu bando zilizowekewa muda wake maalum wa kutumika?