Jenerali Muhoozi Kainerugaba: Kupigana na Rwanda inamaanisha kupigana na Uganda!

Kauli hii inajiri huku mzozo kuhusu wapiganaji wa kundi la M23 ukiendelea.

KWA HISANI
KWA HISANI
Image: Muhoozi Kainerugaba

Mtoto wa kiume wa rais wa Uganda ameibua mjadala tena kwenye mtandao wa kijamii wa Twitter baada ya kutuma ujumbe wenye utata aliouambatanisha na picha ya zamani ya rais wa Rwanda Paul Kagame.

Katika ujumbe huo, Jenerali Kainerugaba amesema:

‘’Mimi ni Jenerali wa nyota 4 wa UPDF (Jeshi la Uganda). Kuna vitu vichache ambavyo sijaviona katika dunia hii. Lakini ninawahurumia wale wanaomdharau mjomba wangu, Jenerali Kagame. Kupigana na Rwanda inamaanisha kupigana na Uganda!

Kauli hii inajiri huku mzozo kuhusu wapiganaji wa kundi la M23 ukiendelea kutokota baina ya Jamuhuri ya kidemokrasi ya Congo na Rwanda.

Congo inaishutumu Rwanda kuwaunga mkono waasi wa M23 walioyateka maeneo mashariki mwa nchi hiyo, madai ambayo Rwanda inayakanusha.

Kwa upande mwingine inaishutumu DRC kwa kushindwa kutimiza ahadi ya kuwarejesha nyumbani waasi wa Rwanda wa kundi la FDLR walioko mashariki mwa DRC inaowashutumu kuhatarisha usalama wa Rwanda.

Hivi karibuni pande mbili zilirushiana cheche za maneno, kila upande ukielezea uwezekano wa kuingia vitani iwapo usalama wake utayumbishwa.

Hii si mara ya kwanza kwa Jenerali Muhoozi kutuma jumbe zenye utata kupitia mtandao wa kijamii kuhusu uhusiano wa nchi yake na nchi jirani, ambazo mara nyingi huibua gumzo mtandaoni, huku baadhi wakijiuliza ni vipi mtu wa kaliba yake anaweza kutoa jumbe za aina hiyo. Katika jumbe zake huwaelezea viongozi wa nchi jirani kama, makaka, na wajomba zake.