Mamia wakimbia ghasia za Sudan Kusini

Mapigano hayo yameenea katika majimbo ya Jonglei na Unity

Muhtasari
  • Siku ya Jumatano, Umoja wa Mataifa ulisema kwamba ghasia hizo zilisababisha vifo vya takribani watu 166

Takriban watu 1,700 wanaokimbia ghasia kati ya makundi yenye silaha katika jimbo la Upper Nile kaskazini wamevuka na kuingia Sudan, shirika la habari la Sudan linalomilikiwa na serikali la Suna limeripoti.

Shirika la Umoja wa Mataifa la Unicef ​​hapo awali lilisema kuwa ghasia kati ya makundi yenye silaha katika jimbo la Upper Nile iliyoanza mwezi Agosti ilikuwa ikilazimisha maelfu ya wanawake na watoto kukimbia makazi yao huku kukiwa na ripoti za kuongezeka kwa vifo vya raia, majeraha na utekaji nyara.

Mapigano hayo yameenea katika majimbo ya Jonglei na Unity. Siku ya Jumatano, Umoja wa Mataifa ulisema kwamba ghasia hizo zilisababisha vifo vya takribani watu 166.

Mjumbe wa Tume ya Misaada ya Kibinadamu ya serikali ya Sudan, Salah Taaj al-Sir, aliiambia Suna kwamba idadi kubwa ya Wasudan Kusini wanaokimbia ghasia wamewasili katika jimbo la mpakani la White Nile.

Ametoa wito kwa makundi ya misaada kutoa msaada wa haraka kwa wakimbizi hao.