Mama wa watoto 7 azaa mapacha 5 kwa mkupuo akitarajia mtoto wa 8

Wasichana 3 na wavulana wawili walikuwa na uzito wa gramu kati ya 710-1400. Walizaliwa na wiki 28.

Muhtasari

• Mama huyo alisema alikuwa anatarajia mtoto wa nane lakini wakaja watano kwa mkupuo badala yake.

Mama apata mapacha 5 kwa mpigo
Mama apata mapacha 5 kwa mpigo
Image: bbc news,

Mwanamke mmoja mama wa watoto saba amepigwa na butwaa baada ya kupata watoto wengine mapacha 5, wakati alikuwa anatarajia mtoto mmoja tu wa nane katika familia yao.

Kulingana na jarida la Manila Times, mwanamke huyo raia wa Poland, mama huyo ambaye tayari alikuwa na watoto saba alipata Baraka hiyo siku ya Jumanne wakati ulimwengu unasherehekea mapenzi.

Dominika Clarke, ambaye tayari ni mama wa watoto saba - ikiwa ni pamoja na jozi mbili za mapacha na ambao umri wao ni kati ya miezi 10 hadi miaka 12 - alijifungua watoto hao watano katika Hospitali ya Chuo Kikuu katika mji wa Krakow, kusini mwa Poland siku ya Jumapili, Manila Times waliripoti.

"Tulipanga kupata mtoto wa nane, lakini ikawa Zaidi. Ikiwa una mfumo, njia ya utulivu na mtazamo mzuri, basi inawezekana kuwa na maisha mazuri sana na kundi kubwa la watoto," aliwaambia waandishi wa habari hospitalini pamoja na mume wake wa Uingereza Vince, kulingana na jarida hilo.

Jarida hilo lilisema kwamba watoto wote watano walikuwa katika afya nzuri na walikuwa na uzito wa mwili kati ya gramu 710 na 1400. Wote walizaliwa kwa njia ya upasuaji wakiwa na wiki 28.

Watoto hao - wasichana watatu na wavulana wawili - waliitwa Arianna Daisy, Charles Patrick, Elizabeth May, Evangeline Rose na Henry James. Clarke aliita ujauzito wake "muujiza," kwani hospitali ilisema uwezekano wa kupata watoto watano ulikuwa mmoja kati ya milioni 52.

Taarifa hizi zinaambatana na zile zilizoripotiwa Kaunti ya Nakuru wiki mbili zilizopita baada ya mwanadada wa miaka 25 kupata watoto 5 kwa mkupuo ila siku moja baadae wakafariki katika hospitali moja mjini Nakuru.