Waumini 80 wakamatwa Ethiopia kinyume cha sheria, walisafiri kukutana na Yesu!

Mchungaji wao aliwahadaa kufunga kwa siku 40 ili kukutana na Yesu siku ya 41, na yeyote ambaye angetaka kukutana na Yesu ni sharti angesafiri hadi Ethiopia.

Muhtasari

• Kabla ya kufunga safari kwenda Ethiopia, mchungaji huyo aliwataka wafuasi wake kuuza mali yao yote.

Image: BBC

Mamlaka za uhamiaji nchini Ethiopia mapema wiki hii waliwakatama raia wa Uganda wapatao 80 ambao walikuwa wameingia nchini humo kinyume cha taratibu za idara za uhamiaji.

Kwa mujibu wa taarifa kutoka Uganda, raia hao walirudishwa katika nchi yao na ilisemekana kwamba walikuwa wamesafiri kwenda nchini Ethiopia katika lengo na azma la kukutana na Yesu.

80 hao walikuwa wameongozwa na mchungaji mmoja kwa jina Pasta Simon Opolot alikuwa amewahadaa waumini wa dhehebu la Christ Disciples Church nchini Uganda kwamba Yesu anapatikana nchini Ethiopia na kuwataka kufunga safari pamoja na yeye ili kukutana naye.

Kabla ya kufunga safari kwenda Ethiopia, mchungaji huyo aliwataka wafuasi wake kuuza mali yao yote kwani walikuwa wanaenda kukutana na Yesu na kuwapeleka moja kwa moja paradiso.

Mchungaji huyo aliwaaminisha wafuasi wake kwamba alipata ufunuo kwa njia ya ndoto kuwa Yesu alikuwa anakuja kuwachukua waja wake, na kuwa wale ambao wangechukuliwa mbinguni ni sharti wangekuwa nchini Ethiopia.

Baada ya kukamatwa nchini Ethiopia, walieleza kuwa lengo lao kuu kule ni kukutana na Yesu na idara ya uhamiaji iliwakusanya wote na kuwarudisha kwao Uganda kwa nguvu.

“Watu hao waliorudishwa wamesema pasta Opolot aliwataka kufunga kwa siku  40 ili wakutane na Yesu siku ya 41. Kigezo kikuu kilikuwa kwamba ili wakutane na Yesu, ni lazima wangeenda Ethiopia na kulingana na yeye, dunia ingeisha baada ya kukutana na Yesu,” mkuu wa idara ya uhamiaji nchini Uganda alinukuliwa.

Hili linakuja miezi kadhaa baada ya mchungaji Paul Mackenzie wa Kenya pia kuwahadaa wafuasi wa kanisa lake la Good News International kwamba wangejinyima chakula na maji ili kukutana na Yesu.

 Kufuatia udanganyifu huo, makumi ya waumini walijinyima chakula na maji hadi kufa ambapo shughuli ya ufukuaji imekuwa ikiendelea katika shamba la Shakahola na Zaidi ya maiti 250 zimefukuliwa.