Afrika Kusini: Watu 16 washukiwa kufariki kutokana na gesi inayoshukiwa kuvuja

Moja ya mitungi ya gesi ilipatikana ikivuja katika mji wa Angelo wenye wakazi wengi wa Boksburg.

Muhtasari

• Waathiriwa walipatikana ndani ya eneo la mita 100 (futi 328) kutoka eneo la tukio.

• Mkasa huu unakuja miezi sita tu baada ya lori la gesi kulipuka katika mkesha wa Krismasi na kusababisha vifo vya watu 41 katika mji huo huo.

Kuna hofu kwamba idadi ya vifo inaweza kuongezeka zaidi.
Kuna hofu kwamba idadi ya vifo inaweza kuongezeka zaidi.
Image: Reuters

Uvujaji wa hewa ya gesi ya nitrate oxide nchini Afrika Kusini unashukiwa kusababisha vifo vya watu 16, maafisa wa eneo hilo wanasema.

Waathiriwa - ikiwa ni pamoja na wanawake na watoto - walikufa baada ya kuvuta gesi kwenye makazi yasiyo rasmi katika eneo la Boksburg, mashariki mwa Johannesburg.

Uvujaji huo uliotokea Jumatano umehusishwa na uchimbaji haramu wa dhahabu katika eneo hilo.

Gesi ya nitrate oksidi mara nyingi hutumiwa na wachimbaji haramu wa dhahabu - wanaojulikana nchini kama zama zamas - kuchimba dhahabu kutoka kwenye udongo ulioibwa kutoka katika mashimo ya migodi yaliyotelekezwa.

Moja ya mitungi ya gesi ilipatikana ikivuja katika mji wa Angelo wenye wakazi wengi wa Boksburg.

Waathiriwa walipatikana ndani ya eneo la mita 100 (futi 328) kutoka eneo la tukio.

Hakuna mtu aliyeweza kupelekwa hospitalini, maafisa wa huduma ya dharura wameambia BBC.

Lakini wanahofia miili zaidi inaweza kupatikana huku timu za uokoaji zikiendelea na kazi yao.

Mkasa huu unakuja miezi sita tu baada ya lori la gesi kulipuka katika mkesha wa Krismasi na kusababisha vifo vya watu 41 katika mji huo huo.