Dhoruba kali yakumba Falme za Kiarabu huku Dubai ikielekeza ndege kwingine

Uwanja wa ndege wa Dubai ulisema shughuli "zilibadilishwa kwa muda" - ingawa zimeanza tena.

Muhtasari

• Mataifa kadhaa yalipata mvua ya takriban mwaka mmoja kwa siku moja.

Mvua kubwa imenyesha katika baadhi ya mataifa ya Ghuba, na kusababisha mafuriko katika eneo hilo na kuzifanya safari za ndege kuelekea uwanja wa ndege wa kimataifa wenye shughuli nyingi zaidi kuelekezwa kwingine.

Uwanja wa ndege wa Dubai ulisema shughuli "zilibadilishwa kwa muda" - ingawa zimeanza tena.

Mamlaka nchini Oman imesema watu 18 wamefariki kutokana na mafuriko.

Mataifa kadhaa yalipata mvua ya takriban mwaka mmoja kwa siku moja.

Video ambayo haijathibitishwa kutoka Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Dubai ilionekana kuonyesha ndege zikiacha mawimbi wakati zikishuka kwenye njia za ndege zilizofurika.

Katika taarifa, uwanja wa ndege ulisema safari za ndege za ndani zilizopaswa kuwasili Jumanne jioni zilielekezwa "kutokana na tukio la hali ya hewa linaloendelea kwa sasa katika UAE".

Safari za kuondoka zitaendelea kama ilivyopangwa, iliongeza. Safari za ndege baadaye zilirejelewa tena baada ya kukatizwa kwa saa mbili.