Raia wa Poland akamatwa kwa kupanga njama ya kumuua rais wa Ukraine

Anaweza kufungwa jela miaka minane ikiwa atapatikana na hatia.

Muhtasari

•Pawel K, alidaiwa kukusanya taarifa kuhusu uwanja wa ndege nchini Poland unaotumiwa na rais wa Ukraine.

Image: BBC

Mwanaume mmoja raia wa Poland amekamatwa na kushtakiwa kwa kupanga kushirikiana na idara za ujasusi za Urusi kusaidia uwezekano wa mauaji ya Rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky, mamlaka ilisema.

Waendesha mashtaka wa Poland walisema mwanamume huyo kwa jina la Pawel K, alidaiwa kukusanya taarifa kuhusu uwanja wa ndege nchini Poland unaotumiwa na rais wa Ukraine.

Kukamatwa kwake kulifanyika kwa msingi wa ujasusi wa Ukraine, waliongeza.

Mamlaka haikubainisha ikiwa mtu huyo kweli alitoa taarifa yoyote.

Anaweza kufungwa jela miaka minane ikiwa atapatikana na hatia.

Mshukiwa yuko chini ya ulinzi na uchunguzi unaendelea.

Katika taarifa, waendesha mashtaka wa Poland walidai Pawel K alikuwa ametoa huduma zake kwa ujasusi wa kijeshi wa Urusi.

Aliwasiliana na Warusi "wanaohusika moja kwa moja katika vita vya Ukraine," waliongeza.

Walisema Pawel K alikuwa amepewa jukumu la kukusanya taarifa kuhusu usalama katika Uwanja wa Ndege wa Rzeszow-Jasionka kusini-mashariki mwa Poland.