Rais mstaafu Uhuru Kenyatta aelezea imani yake na tume ya uchaguzi ya Afrika Kusini

Uhuru ambaye ni mkuu wa tume ya umoja wa Afrika ya waangalizi wa uchaguzi ameelezea imani yake na tume ya uchaguzi ya Afrika kusini huku matokeo rasmi yakitarajiwa kutolewa mwishoni mwa wiki

Muhtasari

•Uchaguzi wa Afrika Kusini ulimalizika Jumatano huku matokeo rasmi yakisubiriwa kutolewa mwishoni mwa wiki.

•Chama cha African National Congress (ANC) kimekuwa madarakani kwa takriban miaka 30 .

Rais mstaafu Uhuru Kenyatta akizungumza na wanahabari,Afrika Kusini
Rais mstaafu Uhuru Kenyatta akizungumza na wanahabari,Afrika Kusini

Rais mstaafu Uhuru Kenyatta amewapongeza raia wa Afrika Kusini kwa uvumilivu wao katika uchaguzi mkuu uliomalizika hivi punde.

Rais huyo mstaafu  ambaye ni mkuu wa tume ya umoja wa Afrika ya waangalizi wa uchaguzi  Alhamisi alihudhuria mkutano fupi kuhusu maendeleo ya uchaguzi mkuu wa IEC uliomalizika hivi majuzi katika kituo cha operesheni ya matokeo katika Kituo cha Mikutano cha Gallagher huko Johannesburg,Afrika Kusini.

Kenyatta alitoa shukrani kwa watu wa Afrika Kusini kwa uvumilivu wao wakati wa ucheleweshaji mkubwa uliopatikana katika mchakato huo. Alipongeza uthabiti wao na kuomba uvumilivu zaidi huku akionyesha imani na uwezo wa tume ya uchaguzi kushughulikia na kutatua masuala yanayoendelea.

Matokeo ya awali yametangazwa kutokana na uchaguzi unaoonekana kuwa wenye ushindani nchini Afrika Kusini tangu chama cha African National Congress (ANC) kiingie madarakani miaka 30 iliyopita. Huku matokeo kutoka takriban asilimia 27  ya wilaya za wapiga kura yamehesabiwa hadi sasa, ANC inaongoza kwa 43%, ikifuatiwa na Democratic Alliance (DA) yenye 25%.

Chama chenye siasa kali za Economic Freedom Fighters (EFF) kina takriban 9%, wakati Chama cha Umkhonto weSizwe (MK Party) cha Rais wa zamani Jacob Zuma ni 8%. Matokeo ya mwisho yanatarajiwa mwishoni mwa wiki.

Aidha matokeo ya awali yanaonyesha kuwa ANC itapoteza wingi wake wa wabunge kwa mara ya kwanza tangu Nelson Mandela kukiongoza chama hicho kupata ushindi kufuatia kumalizika kwa mfumo wa ubaguzi wa rangi mwaka 1994.