Mkutano mkuu wa kuunga mkono uadilifu katika eneo la Ukraine waanza

Urusi haijaalikwa, na mfadhili wake mkuu China hayupo, na kusababisha baadhi ya watu kutilia shaka ufanisi wa mkutano huo.

Muhtasari

•Zaidi ya nchi 90 na mashirika ya kimataifa yanahudhuria mkutano huo

Image: BBC

Viongozi wa dunia katika mkutano wa kilele wa amani wa Ukraine nchini Uswizi wanatarajiwa kupitisha tamko la kuthibitisha uadilifu wa eneo la Kyiv.

Zaidi ya nchi 90 na mashirika ya kimataifa yanahudhuria mkutano huo, unaolenga kuunda uungaji mkono mpana zaidi kuhusu mchakato ambao unaweza kusaidia kumaliza vita nchini Ukraine.

Urusi haijaalikwa, na mfadhili wake mkuu China hayupo, na kusababisha baadhi ya watu kutilia shaka ufanisi wa mkutano huo.

Lakini waliohudhuria, ambao sio wote walio washirika wa karibu wa Ukraine, wanatumai kufikia makubaliano kuhusu masuala kama vile usalama wa nyuklia na mauzo ya chakula nje ya nchi.

Miongoni mwao ni Saudi Arabia, ambayo waziri wake wa mambo ya nje ameonya kwamba Ukraine italazimika kufanya maafikiano magumu, na Kenya, ambayo ilizungumza dhidi ya vikwazo vya hivi karibuni dhidi ya Urusi.

Hata hivyo wajumbe wote wanatarajiwa kuidhinisha taarifa ya mwisho ya kulaani uvamizi wa Urusi.

Rasimu ya waraka huo, iliyoonekana na shirika la habari la Reuters, inataka udhibiti wa Ukraine kurejeshwa kwenye kinu cha nyuklia cha Zaporizhzhia na bandari za nchi hiyo kwenye Bahari ya Azov, zote zinazokaliwa kwa sasa na Urusi.

Pia inarejelea uvamizi wa Urusi kama "vita", nembo ambayo Moscow imeikataa.

Masuala ya kibinadamu kama vile kurejea kwa wafungwa na watoto waliotekwa nyara pia yanajadiliwa.