Mshukiwa katika kesi ya mauaji ya Mirema aachiliwa kwa kukosa ushahidi

Muhtasari
  • Dennis Karani Gachoki aliachiliwa na Hakimu mkaazi wa Milimani Caroline Muthoni baada ya upande wa mashtaka kusema haukuwa na ushahidi wa kutosha
Mshukiwa wa mauaji ya mfanyibiashara Muvota,Dennis Karani
Image: DOUGLAS OKIDDY

Mwanamume mmoja ambaye alishukiwa kuhusika na mauaji ya Samuel Mugoh Muvota huko Mirema, Nairobi, Jumatano asubuhi aliachiliwa na mahakama kwa kukosa ushahidi.

Dennis Karani Gachoki aliachiliwa na Hakimu mkaazi wa Milimani Caroline Muthoni baada ya upande wa mashtaka kusema haukuwa na ushahidi wa kutosha unaomhusisha na mauaji hayo.

"Kwa kuwa hakuna ushahidi kutoka kwa upande wa mashtaka unaomhusisha mshukiwa na mauaji, ninamwachilia na kufunga faili tofauti," hakimu aliamua.

Karani alikuwa amezuiliwa kwa siku 14 akisubiri uchunguzi kufuatia ombi lililofaulu la polisi.

Hata hivyo afisa wa uchunguzi Kapario Lekakeny alizidi kufahamisha mahakama kuwa Karuri alishtakiwa mbele ya mahakama ya Makadara mnamo Jumanne kwa kosa la kuwatia wafanyabiashara wawili dawa za kulevya na kuwaibia pesa taslimu za Sh1.2 milioni.

Anadaiwa kutenda makosa hayo mnamo Juni 24, 2021, katika eneo la MUFU Height kando ya barabara ya Mirema katika kaunti ndogo ya Kasarani kaunti ya Nairobi, pamoja na wengine mbele ya mahakama.

Karani pia anasakwa katika mahakama tofauti kwa kutekeleza uhalifu tofauti.