Barasa kujibu mashtaka ya mauaji chini ya ulinzi mkali Kakamega

Mbunge mteule wa Kimilili Didmus Barasa ameratibiwa kujibu kesi ya mauaji.

Muhtasari

•Barasa ambaye amekuwa akizuiliwa na polisi kwa siku 14 alishtakiwa kwa kumpiga risasi Brian Olunga, msaidizi Brian Khaemba mnamo Agosti 9.

•Uchunguzi wa mwili wa Olunga ulionyesha alikufa kwa risasi ya bastola iliyompiga upande wa kulia wa kichwa chake.

Mbunge Barasa mahakamani
Mbunge Barasa mahakamani

Mbunge mteule wa Kimilili Didmus Barasa ameratibiwa kujibu kesi ya mauaji.

Barasa ambaye amekuwa akizuiliwa na polisi kwa siku 14 alishtakiwa kwa kumpiga risasi Brian Olunga, msaidizi wa mwanasiasa wa Kimilili Brian Khaemba mnamo Agosti 9.

Alizuiliwa katika seli za Kisumu ambapo alihudhuria mahakama kwa njia ya mtandao na polisi kuruhusiwa kumzuilia kwa wiki mbili kabla ya kusikilizwa kwa kesi hiyo mnamo Agosti 24.

Hii ilikuwa kuruhusu polisi kufanya uchunguzi wa mwili wa marehemu na kukusanya ushahidi mwingine unaohitajika kwa kesi hiyo. Pia alifanyiwa vipimo vya afya.

Maafisa walisema angejibu katika mahakama ya Kakamega.

"Hatukuweza kumfungulia mashtaka huko Bungoma kwa sababu za kiusalama," alisema afisa anayefahamu suala hilo.

Uchunguzi wa mwili wa Olunga ulionyesha alikufa kwa risasi ya bastola iliyompiga upande wa kulia wa kichwa chake.

Uchunguzi wa maiti ulionyesha Olunga alikufa kwa kuvuja damu nyingi risasi ilipokwama kichwani mwake.

Risasi ilipatikana. Zoezi hilo liliendeshwa na mtaalamu wa magonjwa eneo la magharibi Dk Dickson Muchana.

Polisi walipewa muda kukamilisha uchunguzi na kuruhusu mashahidi zaidi, wakiwemo maafisa wa NYS na IEBC kurekodi taarifa.

Polisi hadi sasa wameipata bastola ambayo mbunge mteule anadawa kuitumia katika shambulio hilo. Barasa amekana kumpiga risasi mwathiriwa aliyezikwa Jumamosi.

Polisi walisema uchunguzi wa awali umeonyesha kisa hicho kilitokea wakati ugomvi ulipozuka kati ya wawili hao na kumfanya Khaemba kuondoka na kuelekea kwenye gari lake.

"Barasa alimfuata akiwa na wanaume wanne na kuwaamuru wasimruhusu (Khaemba) kuondoka mahali hapo lakini dereva wa Khaemba Joshua Nasokho alikaidi amri hiyo na kuwasha gari," walisema polisi.

Hapo ndipo Barasa alipochomoa bastola na kumlenga msaidizi wa Khaemba Olunga na kumpiga risasi ya paji la uso na kumuua papo hapo.

Alitangazwa kufariki alipofika katika hospitali ya kaunti ndogo ya Kimilili.

Imebainika wawili hao walikuwa na ugomvi siku moja kabla ya kisa hicho cha risasi kutokea.

Timu nyingine ilitumwa eneo hilo kumtafuta mbunge huyo kabla hajajisalimisha.

Mbunge ni mwenye leseni ya kumiliki bunduki.

Awali polisi walikuwa wametoa silaha hiyo lakini mbunge huyo alienda mahakamani na kupata amri ya kurejesha silaha anayoaminika kutumia katika tukio hilo.

Polisi wamepekua mali yake kwa ushahidi zaidi baada ya kupata hati.