Mama wa miaka 58 afungwa jela miaka 29 kwa kumbaka mvulana wa miaka 8

Siku ya tukio, mama huyo ambaye ana watoto hadi na wajukuu alimkuta mtoto akiwa malishoni na kumfanyia kitendo hicho chini ya mti, na kumwambukiza gonjwa la zinaa.

Muhtasari

• Baada ya kuhukumiwa kifungo hicho, hata hivyo wakili wake alisema kuwa walipanga kukata rufaa akisema mteja wake hakufanya hivyo.

• Mama huyo alijitetea akisema ana wajukuu ambao wanamtegemea na hivyo asingepewa adhabu hiyo kali.

Mwanamke aliyefungwa jela pingu mikononi.
Mwanamke aliyefungwa jela pingu mikononi.
Image: Shutterstock

Katika kesi amabyo imekuwa ikifuatiliwa kwa karibu na watu wengi kwa Zaidi ya mwaka mmoja, hatimaye Mahakama ya Wilaya ya Iringa nchini Tanzania imemuhukumu kifungo cha miaka 29 jela mwanamke mmoja ambaye aliripotiwa kumbaka mtoto mdogo.

Mei mwaka jana, vyombo vya habari nchini humo viliripoti kuwa Desderia Mbwelwa akiwa na umri wa miaka 57 kipindi alimbaka mtoto wa kiume mwenye umri wa miaka 8 na kumsababishia magonjwa ya zinaa.

Siku ya tukio mwanamke huyo alimkuta mtoto ambaye ni mwathirika wa tukio hilo akiwa anachunga ng'ombe kisha akamuuliza wenzake walikokuwa na alipojibiwa wenzake hawapo ndipo akambaka akiwa chini ya mti.

Kesi hiyo imesomwa Jumatatu na Hakimu Mkazi Mkuu, Said Mkasiwa na ilikua na mashahidi watano akiwemo daktari aliyempima mtoto na kuthibitisha mtoto huyo alikuwa na michubuko na aliambukizwa magonjwa ya zinaa kutokana na kutokwa uchafu eneo la haja ndogo.

Mahakama ilimpa nafasi ya kujitetea, Desderia alisema yeye ni mtu mzima na kuwa watoto na wajukuu wanaomtegemea, ndipo Mahakama ikamuhukumu kifungo cha miaka 29 jela kwa kosa la ukatili kingono kwa mtoto wa miaka 8 pamoja na kumsababishia magonjwa ya zinaa.

Kulingana na jarida moja la nchini humo, Wakili wake, Frank Mwela alisema kuwa anatarajiwa kukata rufaa kwa kuwa mteja wake hakupimwa ili kubaini kama kweli ana magonjwa hayo ya zinaa.

"Mteja wangu hakupimwa na magonjwa hayo ambaye mteja wangu na shahidi wake wamethibitisha kuwa wao magonjwa hayo hawana kwa sababu shahidi mmoja wapo ni mume wake," amesema.

Desderia ambaye ana miaka 58 ameanza kutumikia kifungo hicho cha miaka 29, huku wakili wake akiendelea taratibu za kukata rufaa.