Khalwale atishia kwenda mahakamani kuhusiana na madai yalioomhusisha na kifo cha mfanyikazi wake

Khalwale ametoa makataa ya saa 48 kwa Shimanyula kuondoa matamshi dhidi yake la sivyo amfikishe mahakamani.

Muhtasari

• Khalwale aliomba kwamba Shimanyulu abatilishe taarifa hizo za kashfa, kwa maandishi, ndani ya saa 48 zijazo.

Dr Boni Khalwale Seneta Kaunti ya Kakamega Picha: HISANI
Dr Boni Khalwale Seneta Kaunti ya Kakamega Picha: HISANI
Image: MAKTABA

Seneta wa Kakamega Boni Khalwale ametishia kwenda mahakamani kudai fidia ya shilingi milioni 200 kutoka kwa mfanyabiashara Cleophas Shimanyula kwa kutoa matamshi ya kumchafulia jina kuhusiana na kifo cha mfanyikazi wake, Kizito Moi.

Khalwale ametoa makataa ya saa 48 kwa Shimanyula kuondoa matamshi dhidi  yake la sivyo amfikishe mahakamani. Seneta huyo alisema kwamba Shimanyula alitoa taarifa za dharau na uongo kwenye mitandao ya kijamii, na kutilia shaka uchunguzi wa polisi kuhusu kifo cha Kizito, ambaye inasemekana aliuawa na fahali mwezi uliopita.

Mapema wiki hii, Khalwale aliwasilisha kesi dhidi ya Shimanyula kwa kudai kwamba alihusika katika kifo cha Moi, licha ya uchunguzi wa maiti kuthibitisha kuwa marehemu aliuawa na fahali.

Katika nyaraka za mahakama, zilizowasilishwa na wakili wake Danston Omari, Khalwale aliomba kwamba Shimanyulu abatilishe taarifa hizo za kashfa, kwa maandishi, ndani ya saa 48 zijazo.

Kulingana na wakili wa Khalwale, iwapo Shimanyalu hatafuata matakwa yaliyoorodheshwa, hatua za kisheria zitachukuliwa dhidi yake.

“Tuna maagizo madhubuti ya kuwasilisha Kesi dhidi yako bila kurejea tena kwako. Bila shaka hii itakuwa katika hatari yako mwenyewe kwa gharama ya fidia kamili na matokeo mengine yanayoambatana nayo,” alisema Omari.

Wiki iliyopita Khalwale alikuwa amedai kuwa wapinzani wake wameingiza siasa katika kifo cha mfanyikazi wake Kizito Moi.

Akizungumza nyumbani kwa marehemu Khalwale aliomba idara husika za serikali kufanya uchunguzi wa kina kubaini kilichomuua Moi.

“Hii si matanga ya Moi, hii ni siasa tupu. Na nataka kushukuru serikali kwa kuona kwamba hii si matanga ni Siasa. Kama haingekuwa siasa Nairobi haingekuwa inakuja hapa. Wako na DCI hapa Malinya, alikuja akafanya kazi yake akamaliza”, Khalwale alisema.

Baada ya matanga Khalwale alikuwa ameahidi kuwakabili wale wote waliongiza siasa kwa mkasa huu.

“Tutamalizana na tutakabiliana wenyewe kisiasa. Nimewakabili hapo nyuma nikawashinda na tena mara hii nitawaibisha”, Khalwale alimalizia.

Marehemu, Kizito Moi kulingana na ripoti iliyowasilishwa na Seneta katika kituo cha polisi cha Malinya alikuwa na umri wa miaka 46 na aliuawa na fahali wake wa kupigana.

Mwili wake ulipatikana kwenye zizi la ng'ombe na mfanyakazi mwingine alipokuwa akizunguka kutekeleza majukumu yake.