Mwanaume ahukumiwa kifo kutokana na wizi wa kimabavu

Tukio hilo lilitokea Juni 23,2023 katika eneo la Kogutu,kaunti ndogo ya Muhoroni,Kaunti ya Kisumu.

Muhtasari

•Kevin Onyango  Kiyogo amehukumiwa kifo  kutokana na wizi wa kimabavu baada ya kumpora James Kamau gari lake aina ya Toyota Hillux lenye thamani Ksh.1,800,000

•Onyango pia anadaiwa kumpa James Kamau madawa ya kulevya kwa nguvu huku akitumikia miaka mitano jela kwa kosa hilo.

•Hukumu ya kifo itasitishwa hadi kukamilika kwa kifungo hicho cha miaka mitano

Mwanaume mmoja amehukumiwa kifo na mahakama ya Tamu iliyoko Muhoroni,kaunti ya Kisumu kwa makosa ya wizi wa kimabavu.

Kevin Onyango Kiyogo amehukumiwa kifo na mahakama ya Tamu kwa mashtaka mawili ya unyang'anyaji kwa  kutumia nguvu kinyume na kifungu cha 296[2]cha kanuni ya adhabu na pia kudanganya ili kutenda kosa kinyume na kifungu cha 230 cha kanuni ya adhabu.

Kulingana na ripoti kutoka kwa afisi ya mkurugenzi wa mashtaka ya umma kenya,mshtakiwa Kevin Onyango Kiyogo alikuwa amejihami kwa silaha hatari.Kwa kutumia vurugu alimpora James Kamau gari lake aina ya Toyota Hillux la thamani ya Ksh 1,800,000.

Vile vile nguli huyo alishtakiwa kwa kumtumia dawa ya kulevya,James Kamau.Makosa hayo yalitekelezwa mnamo  Juni 23,2023 eneo la Kogutu ,kaunti ndogo ya Muhoroni,kaunti ya Kisumu .

Kwenye kesi iliyosikilizwa leo,upande wa mashtaka uliwasilisha ushahidi kupitia mashahidi 8 jambo ambalo mahakama ilikubaliana na kubainisha kuwa vielelezo vyote vilikuwa kweli,hivo Kevin Onyango kupatikana na makosa.

Katika hukumu yake,Hakimu Amos Mokoross alimhukumu mshtakiwa katika shtaka la kwanza la unyang'anyi kwa kutumia nguvu,huku akitumikia adhabu ya kifo.Katika shtaka la pili atatumikia kifungo cha miaka mitano jela.

"Hukumu ya kifo itasitishwa hadi kukamilika kwa kifungo hicho cha miaka mitano." Taarifa kutoka kwa ofisi ya mkurugenzi wa mashtaka ya umma Kenya iliripoti.