Mahakama yaruhusu tume ya EACC kumchunguza Kidero

Kidero anakabiliwa na madai ya rushwa na uhalifu wa kiuchumi akihudumu kama gavana wa kaunti ya Nairobi

Muhtasari

• Mahakama ya rufaa imeiruhusu tume ya EACC kuchunguza akaunti za benki zinazohusishwa na gavana huyo wa zamani.

• Kidero amepata pigo kwa mara ya pili baada ya mahakama ya juu,mwaka wa 2016 kutupilia mbali rufaa aliyowasilisha katika mahakama hiyo

KIDERO-1
KIDERO-1

Gavana wa zamani wa kaunti ya Kakamega Evans Kidero amepata pigo baada ya mahakama ya rufaa kutupilia mbali ombi lake la kutaka EACC kuwacha kuchunguza akaunti zake za banki.

Benchi la majaji watatu lilitupilia mbali ombi la Kidero mnamo Ijumaa tarehe 20.

Kidero alishtakiwa na tume ya maadili na kupambana na ufisadi EACC kwa madai ya rushwa, uhalifu wa kiuchumi na kupata mali kwa njia mabzo hakuziweka wazi.

Mwaka wa 2016, Kidero aliwasilisha rufaa katika mahakama ya juu akiitaka mahakama hiyo kuizuia EACC kuendelea na uchunguzi wa madai ya ufisadi dhidi yake.

Tume ya EACC, wakati huo ilikuwa imepokea vibali kutoka kwa mahakama ya hakimu mkuu ya kuendelea kufanya uchunguzi kwa akaunti za banki zinazohusishwa na Kidero.

Madai ya ufisadi dhidi ya Kidero yanahusishwa na wakati wake akiwa gavana wa kaunti ya Nairobi sawia na meneja wa usimamizi wa kampuni ya kusaga miwa ya Mumias.

Rufaa hiyo ya Kidero ya mwaka 2016 kwa mahakama ya juu, aidha ilifutiliwa mbali na majaji George Vincent Odunga, Chacha Mwita na John Mativo mnamo tarehe 8 Juni mwaka wa 2018.

Kidero katika rufaa yake kwa mahakama ya rufaa, alisema kuwa vitengo kadhaa katika sheria ziliipa EACC uwezo wa kufanya uchunguzi kinyume na sheria.

Vile vile, alilalamika kuwa EACC kufanya uchunguzi katika akaunti zake za banki ilikuwa tisho kwa haki zake za kimsingi na uhuru wake.

Sasa, EACC imepewa rukhsa ya kuendelea kumchunguza Kidero.