Kwa nini Jenerali Francis Ogolla atazikwa bila jeneza

Marehemu alikuwa amemuonyesha mahali halisi pa kaburi lake; karibu na nyumba yake katika kijiji cha Mor, Kaunti ya Siaya.

Muhtasari

•Oduor alisema mazishi yatakuwa rahisi sana na kwa kuzingatia matakwa ya marehemu Jenerali atazikwa ndani ya saa 72 baada ya kifo chake.

•Dadake Jenerali, Peris Onyango, alizungumza na Radio Jambo na kutaja kwamba kakake alikuwa amejitayarisha sana kwa kifo.

Jenerali Francis Ogolla
Jenerali Francis Ogolla
Image: HISANI

Marehemu Jenerali Francis Ogolla atazikwa bila jeneza kuheshimu matakwa yake, kakake mkubwa Canon Hezekiah Oduor amesema.

Oduor alisema mazishi yatakuwa rahisi sana na kwa kuzingatia matakwa ya marehemu Jenerali atazikwa ndani ya saa 72 baada ya kifo chake.

Alisema zaidi kwamba kaka yake alikuwa amemuonyesha mahali halisi pa kaburi lake; karibu na nyumba yake katika kijiji cha Mor, Kaunti ya Siaya.

Oduor alisema mazishi yatafanyika Jumapili, Aprili 21.

Marehemu Jenerali Ogolla alifikiria mazishi rahisi sawa na mila ya Waislamu, matakwa ambayo familia ilisema aliandika katika Wosia wake.

Kulingana na maagizo ya Ogolla, mwili wake unapaswa kufungwa kwa shuka, uamuzi uliofanywa ili kupunguza kile alichotaja kuwa shinikizo lisilo la lazima kwa familia.

Lakini licha ya unyenyekevu wa mazishi, familia ilifichua kuwa mila zingine za Wajaluo zitazingatiwa.

Oduor alitoa mwaliko kwa wale wanaotaka kuomboleza pamoja nao wajiunge ama kiroho au kimwili, akihakikisha kwamba kutakuwa na chakula cha kutosha kwa wageni wote.

Dadake Jenerali, Peris Onyango, alizungumza na Radio Jambo na kutaja kwamba kakake alikuwa amejitayarisha sana kwa kifo.

Alisema wakati wowote angemtembelea, angemweleza jinsi mazishi yake yanapaswa kuonekana, licha ya majaribio yake ya kumzuia kutoka kwa mawazo kama hayo.

Onyango aliongeza kuwa kakake alisisitiza mara kwa mara kuwa kifo ni ukweli, hasa kwa wanajeshi kama yeye ambao hutazama kifo usoni wakiwa kazini.

"Kifo cha ghafla kimesababisha jamii nzima katika hali ya sintofahamu kwani Ogolla alikuwa mfadhili," Onyango alisema.

Alimtaja marehemu kaka yake kuwa mkarimu sana na mtu aliyesikiliza matatizo yanayowakumba wanakijiji.

"Alisaidia kanisa na kuhakikisha kukamilika kwake, alitoa kisima cha maji, na alizawadia shule alizosoma.

"Ndio maana taarifa za kifo chake zilipoibuka jana, watu walikuja kwa wingi kumuomboleza kwa sababu hakuwa na mipaka," alisema.

Hata hivyo, familia ilisisitiza kuwa sherehe za kuadhimisha miaka 100 ya kuzaliwa kwa baba yao Mzee Joel Oyeyo, zitaendelea jinsi ilivyopangwa Jumamosi.

Familia hiyo ilikuwa imepanga kusherehekea siku ya kuzaliwa ya centinerian siku ya Jumamosi na kuwekwa wakfu katika Kanisa la Anglikana la St Thomas Nduru siku ya Jumapili.

Jenerali Ogolla alipaswa kusafiri hadi kijijini kusaidia matayarisho ya hafla zote mbili Ijumaa hii, familia ilifichua.