Nitakumiss sana Mama Mia! Robert Nagila amuomboleza mpenzi wake Rita Tinina

Nagila alibainisha kuwa kifo cha Tinina ni pengo ambalo haliwezi kuzibika

Muhtasari
  • Nagila pia alizungumzia jinsi kifo cha Tinina kilivyoathiri maisha ya watu wengi jambo ambalo lilithibitishwa na watu waliokuwepo kwenye misa hiyo.
  • Akimwangalia Mia Malaikah ( binti yake na Tinina), Nagila alisema kwamba alipendwa sana na mama yake.
Mumewe Rita Tinina, Robert Nagila
Image: Enos Teche

Robert Nagila, mpenzi wa marehemu mwandishi wa habari Rita Tinina ameshiriki ujumbe mzito kutoka moyoni kuhusu jinsi Tinina ameacha u.

Akizungumza Jumatatu, Nagila alianza hotuba yake kwa kumpa Tinina maua zake.

"Cha kushangaza ni kwamba Rita alianzisha kumbukumbu yake, baada tu ya siku yake ya kuzaliwa ya 46," alisema.

Nagila pia alizungumzia jinsi kifo cha Tinina kilivyogusa maisha ya watu wengi jambo ambalo lilithibitishwa na watu waliokuwepo kwenye misa hiyo.

Aliendelea  kusema kwamba katika wiki iliyopita, imebidi asome na atazame heshima nyingi kwa mwanamke wa kipekee ambaye Tinina alikuwa.

Akikumbuka nyakati fulani, Nagila aliwasimulia waombolezaji kuhusu pale alipokutana na Tinina.

"Njia zetu zilipokutana kwa mara ya kwanza , kicheko na moyo mchangamfu vilinigusa. Lakini pia wewe ndiye mtu mkaidi zaidi niliyewahi kukutana naye," alisema.

"Nitakumiss sana, Mama Mia."

Nagila alibainisha kuwa kifo cha Tinina kilikuwa pengo ambalo haliwezi kuzibika.

"Jumapili iliyopita, simu yako iliacha kuita. Kukufa kwako kumeacha pengo ambalo haliwezi kuzibika. Lakini nimefarijiwa na ukweli kwamba kumbukumbu za muda uliotumika zitabaki nasi," aliongeza.

Akimwangalia Mia Malaikah ( binti yake na Tinina), Nagila alisema kwamba alipendwa sana na mama yake.

"Mia mpenzi wangu, mama yako alikupenda kuliko kitu  chochote katika ulimwengu huu. Ulikuwa rafiki yake mkubwa na msiri wake," alisema.

"Na kila jambo alilofanya lilihusu wewe na maisha yako ya baadaye. Jua hili, Unapendwa sana na hakuna jambo ambalo tusingefanya kwa ajili yako."

Kwa familia, Nagila aliangazia kwamba mwanahabari marehemu aliwachukulia kwa heshima kubwa na familia ndio ilikuwa kitovu cha maisha yake.

Kwa kuongezea, Nagila alitoa shukrani zake kwa marafiki wa Tinina na udungu wa wanahabari kwa usaidizi wa dhati waliouonyesha kwa familia.

Kabla ya maziko siku ya Jumatano, alisema kuwa watu wanapaswa kusherehekea maisha ya Tinina hata wanapomlaza.

"Ni maombi yangu tunaposafiri kwenda Narok, na nasema haya kwa moyo mzito sana, tuwe na kwaheri ya mwisho ya  kusherehekea maisha yake," Nagila aliongeza.

Tinina atazikwa Jumatano, Machi 27 katika kaunti ya Narok nyumbani kwa familia, Noosupeni Farm Olokirikirai.

Tangazo la kifo na mazishi lililoonekana na The Star lilisema Tinina binti mpendwa wa marehemu Dominic na marehemu Mary Yiapan.

"Alikuwa mamake Mia Malaikah na mpenzi wake Robert Nagila," lilisoma tangazo hilo.

"Pia alithaminiwa sana kama dada-mkwe wa Timothy, Roshen, Belmont, Agnes na Macharia."

Alikuwa dada mpendwa wa Helen, Irene, Justine, Jedidah, Keen na Claudia.