Rais William Ruto ajawa bashasha baada ya kupokea Kombe la EPL katika Ikulu (+picha)

Rais Ruto pia alichukua muda kuonyesha ujuzi wake wa soka kwa maafisa wa soka waliowasilisha kombe hilo katika ikulu.

Muhtasari

•Rais alipongeza ligi ya Uingereza kwa kuwa makao ya muda ya Victor Wanyama na mwanawe Mike Origi, Divork Origi.

•Rais wakati huo huo alibainisha kuwa Ligi ya Uingereza imewatia moyo na kuwavutia wanasoka wengi kutoka bara la Afrika.

alipokea Kombe la EPL katika ikulu mnamo Septemba 3, 2023.
Rais William Ruto alipokea Kombe la EPL katika ikulu mnamo Septemba 3, 2023.
Image: PSC

Rais William Samoei Ruto amefunguka kuhusu furaha yake kubwa baada ya kupokea kombe la Ligi Kuu ya Uingereza katika Ikulu ya Nairobi.

Katika taarifa yake Jumapili asubuhi, rais alipongeza ligi ya Uingereza kwa kuwa makao ya muda ya nahodha wa zamani wa Harambee Stars Victor Wanyama na Divork Origi wa Nottingham ambaye ni mwana wa mwanasoka wa zamani wa Kenya Mike Origi.

Kombe hilo liliwasilishwa kwa ikulu ya Nairobi na nguli wa soka wa Nigeria Jay-Jay Okocha na maafisa wengine wa EPL.

“Nimefurahi kukaribisha Kombe la Ligi Kuu ya Uingereza katika Ikulu ya Nairobi. Kombe hilo lilisindikizwa na nguli wa soka Jay-Jay Okocha. Ligi hiyo imemkaribisha nahodha wa zamani wa Harambee Stars, Victor Wanyama, ambaye alichezea Southampton na baadaye Tottenham Hotspurs na Divock Origi (zamani Liverpool), mtoto wa nyota wa zamani wa Stars Mike Origi,” Rais Ruto alisema katika taarifa.

Zilizoambatanishwa na taarifa hiyo ni picha za amri jeshi mkuu huyo akikaribisha kombe hilo la kifahari kwenye ikulu. Pia alichukua muda kuonyesha ujuzi wake wa soka kwa wasimamizi hao wa soka.

Rais wakati huo huo alibainisha kuwa Ligi ya Uingereza imewatia moyo na kuwavutia wanasoka wengi kutoka bara la Afrika.

“Ligi ni msukumo kwa mamilioni ya wanasoka chipukizi kote ulimwenguni; Afrika, Kenya pamoja. Ni mwishilio wa mwisho wa soka,” alisema.

Ruto alibainisha kuwa soka ni shughuli kubwa ya kibiashara na kutoa wito wa usimamizi mzuri wa mchezo huo nchini ili kutumia uwezo wake.

"Uwezo wa kibiashara wa kandanda ya kulipwa ni mkubwa vya kutosha kuhamasisha vipaji vingi vijavyo, kubadilisha maisha ya maelfu ya wachezaji, makocha na jamii. Lazima tusimamie mchezo ipasavyo ili kukuza na kutumia uwezo huu,” alisema.

Kombe la EPL limekuwa humu nchini tangu siku ya Ijumaa ilipoanza ni ziara ya siku tatu ya Nairobi inayokamilika leo, Septemba 3.