Askari ashtakiwa kwa kusababisha madhara makubwa kwa mkewe mjamzito

Muhtasari
  • Kulingana na ripoti ya polisi, askari alienda nyumbani akiwa amelewa na kumshambulia mkewe
  • Mtuhumiwa alikamatwa na kufunguliwa mashtaka mahakamani
Image: Clause Masika

Afisa wa polisi Ijumaa alishtakiwa katika mahakama ya Kibera kwa madai ya kumpiga mkewe mjamzito wa miezi mitatu na kumpoteza mtoto wake.

Ernest Muriungi alishtakiwa mbele ya hakimu wa mahakama ya Kibera William Tulel ambapo alikanusha mashtaka na kuitaka mahakama kumwachilia kwa dhamana nafuu ya pesa taslimu.

Anadaiwa kutenda kosa hilo mnamo Oktoba 21 katika gereza la wanawake la Lang’ata katika kaunti ndogo ya Lang’ata ndani ya Kaunti ya Nairobi.

Kulingana na ripoti ya polisi, askari alienda nyumbani akiwa amelewa na kumshambulia mkewe.

Taarifa za polisi zinasema kuwa mwanamke huyo ambaye alikuwa mjamzito alianza kuvuja damu na kukimbizwa katika hospitali ya karibu ambako alihudumiwa na baadaye kufahamishwa kuwa alipoteza mtoto wake wa miezi mitatu.

Mtuhumiwa alikamatwa na kufunguliwa mashtaka mahakamani.

Ijumaa katika mahakama wakili wa serikali Robert Ogallo aliitaka mahakama kumwachilia kwa dhamana ya juu kwani kosa alilotenda lilikuwa na madhara makubwa.

Ogallo aliambia mahakama kuwa masuala ya unyanyasaji wa kijinsia yameongezeka katika siku za hivi majuzi kwa hivyo kesi hiyo ilihitaji kuzingatiwa kwa uzito.

"Katika siku za hivi karibuni tumeona masuala ya ukatili wa kijinsia yameongezeka. Naomba mahakama hii tukufu izingatie pia kwamba kosa lililofanyika ni kosa kubwa," aliiambia mahakama.

Ogallo aliambia mahakama kuwa alikuwa tayari kumpatia mshtakiwa taarifa za shahidi na ushahidi wa maandishi. Aliiambia mahakama kuwa mshitakiwa ni mkosaji wa mara ya kwanza na kuitaka ifanye maamuzi yake katika masuala yanayohusu utoaji wa masharti ya dhamana.

Tulel alimwachilia kwa dhamana ya Sh20,000 pesa taslimu na bondi ya Sh100,000.

Mahakama iliagiza kesi hiyo itajwe Novemba 12 kwa maelekezo zaidi.