Katombi watumbuliwa

Muhtasari

• Kundi la kigaidi nchini Kenya almaarufu Katombi Gang limepata pigo kubwa baada ya njama yao ya uhuni kutibuliwa na polisi jijini Nairobi.

• Fadhili Mgaza ambaye amekuwa ni jambazi sugu wa kundi la Katombi alipatana na umauti wake wakati alidinda kutii amri ya kusalimisha silaha kwa polisi

Tukio la kigaidi
Tukio la kigaidi
Image: HISANI

Kundi la kigaidi nchini Kenya almaarufu Katombi Gang limepata pigo kubwa baada ya njama yao ya uhuni kutibuliwa na polisi jijini Nairobi.

Mmoja wa wahuni wa kundi hilo ambalo limekuwa likiwahangaisha wakaazi jijini alisafirishwa jongomeo na maafisa wa polisi waliokuwa wakipiga doria wakati walivamia magaidi hao wakiwa katika harakati ya kudai vitu visivyo vyao.

Fadhili Mgaza ambaye amekuwa ni jambazi sugu wa kundi la Katombi alipatana na umauti wake wakati alidinda kutii amri ya kusalimisha silaha kwa polisi na hivyo kuzua mchezo wa nzi na fisi kwenye mzoga, jambo ambalo lilipelekea wanadoria kumfyatulia risasi na kumuuwa.

Ripoti za upelelezi zinasema jambazi huyo alikuwa miongoni mwa wanne ambao walikwepa mtego wa polisi mwezi Desemba mwaka uliopita mtaani Mathare lakini safari hii kuzimu ilimpa tabasamu na kumuita.

DCI wanasema kwamba wanne hao mwishoni mwa mwaka jana walijaribu kutekeleza windo lao haramu kwa wananchi katika barabara ya Mau Mau ila polisi wakawahi kwa wepesi mno na kutibua njama hiyo katika kisa ambapo kiongozi wa kundi hilo, Ngaruiya alipewa pasipoti ya kusafiri moja kwa moja kuelekea kuzimuni kwa mtutu wa bunduki za polisi huku Mgaza na wenzake wakiponea kwa kujitoma katika maji taka na kupiga mbizi mithili ya Kambare atorokaye ndoana ya mvuvi.

Ila safari hii mtego wa polisi ulikuwa ange kabisa kwani alivumaniwa akifanya uhalifu wake katika eneo la Mlango Kubwa mtaani Mathare ambapo alianza kufyatulia polisi risasi ila mbio zake za sakafuni zikalazimika kuishia ukingoni baada ya polisi wenye tajriba iliyotukuka kumshinda katika tukio hilo na kumuua.

Kundi la Katombi sasa limesalia bila kiongozi baada ya viongozi wao wawili kubusu mtutu wa bunduki za polisi chini ya miezi miwili.