Mwanamume mahakamani kwa wimbo unaohusisha gavana na vifo vya wabunge watatu

Muhtasari
  • Mwanamume mahakamani kwa wimbo unaohusisha gavana na vifo vya wabunge watatu
Mahakama
Mahakama
Image: MAKTABA

Mwanamume mmoja ameshtakiwa kortini kwa kutoa wimbo unaoonyesha kuwa Gavana wa Marsabit Mahammud Ali alihusika na vifo vya waliokuwa wabunge watatu wa Moyale.

Jarso Wako alishtakiwa kwa kutunga na kutoa wimbo huo ambao kulingana na upande wa mashtaka ulibeba maneno ambayo huenda yakazua wasiwasi kwa umma.

Hususan ya shtaka kama ilivyoonyeshwa kwenye karatasi ya mashtaka ni "kujiendesha kwa njia inayoweza kusababisha uvunjifu wa amani"

Galma Godana, Guyo Halake na Dkt. Guracho Galgalo wote walihudumu kama Wabunge katika Eneo Bunge la Moyale.

Godana alipigwa risasi na kufa mwaka wa 2015 katika kisa cha wizi nyumbani kwake Syokimau, Machakos. Halake kwa upande mwingine alipigwa risasi na washambuliaji wasiojulikana nyumbani kwake Moyale mnamo 2014 naye Dkt Guracho alifariki katika ajali ya ndege ya Marsabit 2006.

Wako ambaye alifika mbele ya Hakimu Mkuu Wendy Michenj alikanusha shtaka hilo na kuachiliwa kwa dhamana ya pesa taslimu Sh100,000.

Watu wawili wameorodheshwa kama mashahidi katika kesi hiyo.

Kesi hiyo itasikizwa Mei 11.