Sakaja aamuru kuachiliwa kwa pikipiki zilizokamatwa Nairobi

Sakaja alisema pikipiki hizo zinapaswa kutolewa kwa wamiliki na kesi zote ziondolewe mara moja.

Muhtasari

• Sakaja alikuwa akizungumza wakati wa mkutano na Wafanyakazi wa Kaunti hiyo.

Johnson Sakaja, akihutubia wanahabari
Johnson Sakaja, akihutubia wanahabari
Image: RADIO JAMBO

Gavana wa Nairobi Johnson Sakaja ameamuru pikipiki zote zilizoshikwa na kaunti ya Nairobi ziachiliwe.

Sakaja alisema pikipiki hizo zinapaswa kutolewa kwa wamiliki na kesi zote ziondolewe mara moja.

Akitoa maagizo hayo siku ya Jumatatu, Sakaja pia aliitaka idara ya ukaguzi ya Jiji kubainisha maeneo rasmi ya uchukuzi na ushushaji wa abiria kati kati mwa jiji la Nairobi.

Sakaja alikuwa akizungumza wakati wa mkutano na Wafanyakazi wa Kaunti hiyo.

Mnamo Julai, Nairobi Metropolitan Services walisema wanapanga kuachilia pikipiki zote za bodaboda zilizozuiliwa Nairobi kabla ya uchaguzi.

Mkurugenzi Mkuu wa NMS Mohammed Badi alisema atashauriana na Inspekta Jenerali wa Polisi Hillary Mutyambai kuhusu suala hilo.

"Baadhi ya bodaboda walikuwa wamezuiliwa, nitashauriana na IG na kuhakikisha wanaachiliwa kabla ya uchaguzi," alisema.

Badi alikiri kuwa waendeshaji bodaboda wamekuwa waathiriwa wa maafisa wa kutekeleza sheria walaghai.

“Tangu nichukue Nairobi nimefanya kazi kwa karibu na vyama vya boda boda. Ni kweli waendeshaji bodaboda wamekuwa wakinyanyaswa na maafisa wa kutekeleza sheria walaghai."

Badi alisema ameanzisha hatua za kinidhamu dhidi ya maafisa hao wabadhirifu na atawafuta kazi.

Kwa kufuata maagizo ya Sakaja, NMS haikuweza kutoa pikipiki hizo kwa wamiliki.