Watu 3 wafariki baada ya ukuta wa mchanga kuwaangukia Machakos

Wote Nzilani na Makau wanatoka eneo la Kitulu huku Kapee akiripotiwa kuwa mkazi wa kaunti ndogo ya Kathiani.

Muhtasari
  • Polisi waliiondoa miili hiyo hadi katika chumba cha kuhifadhi maiti cha Hospitali ya Machakos Level 5 baada ya wakaazi kusaidia katika kupatikana kwao

Watu watatu wamefariki walipokuwa wakichimba mchanga katika kaunti ya Machakos.

Watatu hao walifariki baada ya ukuta wa machimbo waliyokuwa wakichimba mchanga kuporomoka katika kijiji cha Kithatani, Kivandini, eneo la Mvuti kaunti ndogo ya Machakos mnamo Alhamisi.

Kamanda wa polisi wa kaunti ndogo ya Machakos Moss Ndhiwa alisema wawili kati ya waathiriwa walifariki papo hapo huku mwengine akitangazwa kufariki alipofika katika hospitali ya Machakos Level 5.

"Watatu hao walikuwa wakichimba mchanga katika eneo lenye kina kirefu wakati ukuta wake ulipoporomoka na kuwazika wakiwa hai. Wawili walifariki papo hapo na mwingine alifariki dunia katika Hospitali ya Machakos Level 5," Ndhiwa alisema.

Walitambuliwa na wakaazi kama Musyoka Nzilani, 19, Mutinda Makau, 32, huku wa tatu akijulikana tu kama Masaku almaarufu Kapee, 40.

Wote Nzilani na Makau wanatoka eneo la Kitulu huku Kapee akiripotiwa kuwa mkazi wa kaunti ndogo ya Kathiani.

Ndhiwa aliwaonya wakazi hao dhidi ya kujihusisha na vitendo hivyo akieleza kuwa ni hatari.

"Nataka kuwatahadharisha wakazi wa Machakos dhidi ya kuvuna mchanga katika maeneo hatarishi kama haya. Hakuna mtu anayepaswa kuhatarisha maisha yake kwa kujitafutia riziki. Tumepoteza maisha ya watu watatu. Hili halikubaliki, hatutaruhusu zaidi matukio kama haya yatapona," Ndhiwa alisema.

Polisi waliiondoa miili hiyo hadi katika chumba cha kuhifadhi maiti cha Hospitali ya Machakos Level 5 baada ya wakaazi kusaidia katika kupatikana kwao.