Seneti kuamua hatima ya gavana Mwangaza mnamo Desemba 30

"Ilani inatolewa kwa Maseneta wote kwamba nimewateua Ijumaa, tarehe 30 Desemba, 2022, kama siku ya kikao maalum cha Seneti.

Muhtasari
  • Haya ni kulingana na spika wa seneti Amason Kingi anayesema kuwa kikao hicho kinachotarajiwa kufanyika saa 2:30 jioni
GAVANA WA MERU KAWIRA MWANGAZA
Image: EZEKIEL AMING'A

Bunge la Seneti tarehe 30 Desemba 2022, litafanya kikao maalum kujadili hatma ya Gavana wa Meru Kawira Mwangaza.

Haya ni kulingana na spika wa seneti Amason Kingi anayesema kuwa kikao hicho kinachotarajiwa kufanyika saa 2:30 jioni kitatanguliwa na kuapishwa kwa seneta mteule wa Bungoma David Wakoli.

"Ilani inatolewa kwa Maseneta wote kwamba nimewateua Ijumaa, tarehe 30 Desemba, 2022, kama siku ya kikao maalum cha Seneti. Kikao hicho kitafanyika katika Ukumbi wa Seneti, Majengo ya Bunge Kuu, Ghorofa ya Chini, Nairobi, kuanzia saa 2.30 p.m," Kingi alisema kwenye notisi ya gazeti la serikali.

"Kwa mujibu wa kanuni ya kudumu ya 33(5) ya Kanuni za Kudumu za Seneti, shughuli iliyotajwa katika Notisi hii itakuwa shughuli pekee mbele ya Seneti wakati wa kikao maalum, baada ya hapo, Seneti itasitishwa hadi Jumanne, Februari 14, 2023, saa 2.30 asubuhi wakati Seneti itaendelea na vikao vyake vya kawaida kwa mujibu wa Kalenda ya Seneti. Tarehe 28 Desemba 2022."

Gavana Mwangaza kwa sasa anakabiliwa na kuondolewa madarakani baada ya wabunge 68 wa Meru, mnamo Oktoba, kuunga mkono hoja iliyopendekezwa na MCA wa Abogeta Magharibi Dennis Kiogora ya kumshtaki kwa msingi kwamba alikuwa amekiuka mamlaka yake ya kikatiba.