Umati wa watu wavamia kituo cha polisi, wamuua mshukiwa na kuchoma mwili wake Kapenguria

Kirui aliwataka wenyeji kuwaachia polisi kushughulikia masuala hayo, akiwaonya dhidi ya kuchukua sheria mkononi.

Muhtasari
  • Alikuwa amekamatwa kwa madai ya kumuua mwanafunzi wa shule ya upili ya Pser na kutupa mwili wake katika eneo la Cherangany siku chache zilizopita.
  • Marehemu pia anashukiwa kuwa mwanachama wa genge linaloaminika kuiba pikipiki na kuua watu mjini humo.
Crime Scene
Image: HISANI

Mwanamume mmoja alishambuliwa, kuuawa na kuchomwa moto Jumatano jioni katika kituo cha Polisi cha Makutano huko Kapenguria, Pokot Magharibi.

Shambulizi hilo lilitokea wakati polisi wakijiandaa kumhamishia mshukiwa  katika kituo cha polisi cha Kapenguria.

Alikuwa amekamatwa kwa madai ya kumuua mwanafunzi wa shule ya upili ya Pser na kutupa mwili wake katika eneo la Cherangany siku chache zilizopita.

Marehemu pia anashukiwa kuwa mwanachama wa genge linaloaminika kuiba pikipiki na kuua watu mjini humo.

OCPD wa Kapenguria Kipkoech Kirui alisema walijaribu kuzuia umati huo bila mafanikio, akiongeza kuwa maafisa walijeruhiwa wakati wa ghasia hizo.

Akisimulia kisa hicho, OCPD alisema kundi la watu wapatao 700, waliokuwa wamekusanyika karibu na kituo hicho walimvuta kwa nguvu mshukiwa alipokuwa akipanda Toyota Land cruiser.

"Walianza kumpiga mara moja kwa kutumia mawe na vipande vya mbao hadi akafa umbali wa mita 100 kutoka kwenye nguzo," alisema.

"Polisi walijaribu kujizuia lakini umma waliwazidi nguvu polisi. Katika harakati hizo, maafisa walipata majeraha kama ifuatavyo: Cpl Ali Mohammed alipigwa kifundo cha mkono wa kushoto na pia simu yake ya mkononi iliyotengeneza Techno 19 yenye thamani ya Sh24,000 iliporwa, Pc Bare Aden alipoteza. jino moja na Pc Juma Dalo alijeruhiwa kwenye mbavu za kulia na magoti yote."

Kirui aliwataka wenyeji kuwaachia polisi kushughulikia masuala hayo, akiwaonya dhidi ya kuchukua sheria mkononi.

"Ikitokea mtuhumiwa yeyote toa taarifa tu kwa polisi, tutoe ushirikiano kwa sababu tunajaribu kukomesha wizi," alisema.

Shuhuda wa tukio hilo aliwataka vijana hao kutafuta ajira zikiwemo za hali ya chini ili kuwaweka bize na kujikimu kimaisha.

Mwili huo umehamishwa hadi katika chumba cha kuhifadhi maiti cha hospitali ya rufaa ya Kaunti ya Kapenguria ukisubiri uchunguzi wa maiti.