Huduma za afya za lemazwa katika kaunti nne kufuatia mgomo wa madaktari

Atellah alisema kuwa kaunti tatu za Bomet, Mombasa na Nyandarua zimewasiliana na muungano huo na kuahidi kulipa

Muhtasari
  • Mnamo Jumatano, Aprili 19, madaktari wa Vihiga na Nyamira waliingia barabarani kutaka kuketi na serikali zao za kaunti.

Huduma za afya katika kaunti nne zimelemazwa kufuatia mgomo wa madaktri katika kaunti hizo.

Madaktari kutoka Kaunti za Bomet, Kisumu Nyamira na Vihiga, wanalalamika kucheleweshwa kwa mishahara kwa miezi kadhaa iliyopita.

Mnamo Jumatano, Aprili 19, madaktari wa Vihiga na Nyamira waliingia barabarani kutaka kuketi na serikali zao za kaunti.

 

“Familia zetu ziko nyumbani zikihangaika. Watoto wetu hawawezi kwenda shule na wengi wetu hatuwezi kulipa karo kwa wakati ufaao ilhali tuko mstari wa mbele kusaidia wengine,” alisema muuguzi katika Kaunti ya Nyamira.

Katika kaunti ya Kisumu, wagonjwa walihudumiwa na wanafunzi wa udaktari huku wale waliohitaji huduma maalum wakisalia kukwama.

Katibu Mkuu wa Muungano wa Madaktari, Wafamasia na Madaktari wa Meno nchini (KMPDU) Dkt Davji Atellah anasema madaktari na wahudumu wote wa afya huko Nyamira, Vihiga na Kisumu watasalia nyumbani hadi matakwa yao yatimizwe.

Atellah alisema kuwa kaunti tatu za Bomet, Mombasa na Nyandarua zimewasiliana na muungano huo na kuahidi kulipa. Alisema kaunti zina hadi mwisho wa juma kutimiza ahadi yao.

“Hakuna kiasi cha vitisho ambavyo kaunti zitajaribu ambazo zitasuluhisha matokeo ya wafanyikazi kupata haki zao. Ni jukumu la serikali ya kaunti kuwalipa na kuwatunza wafanyikazi wao,” akasema Atellah.

Katika notisi kwa machifu 12 wa kaunti siku ya Jumamosi, matabibu kutoka miungano mbalimbali ya afya walisema hawawezi kukidhi mahitaji yao ya kila siku na hivyo basi, hawawezi kuripoti kazini.