Polisi wazuia wanahabari kunasa matukio ya ufukuzi wa maiti Shakahola

Kufikia Jumatano, shughuli ya ufukuzi wa maiti ilikuwa imechukua siku sita na zaidi ya miili 90 kufukuliwa.

Muhtasari

•Haijulikana kama asasi za usalama zitaendelea kutoa sasisho kuhusu shughuli ya ufukuzi kwa umma kupitia vyombo vya habari.

waanza kuopoa miili ya watu wanaoaminika kuwa wafuasi wa kasisi wa Malindi Paul Mackenzie katika eneo bunge la Shakahola Magarini kaunti ya Kilifi.
Maafisa wa upelelezi kutoka kitengo cha mauaji na wataalam wa uchunguzi waanza kuopoa miili ya watu wanaoaminika kuwa wafuasi wa kasisi wa Malindi Paul Mackenzie katika eneo bunge la Shakahola Magarini kaunti ya Kilifi.
Image: ALPHONSE GARI

Jumatano ikiwa ni siku ya sita tangu shughuli za ufukuzi wa maiti katika shamba la mchungaji mwenye itikadi potovu Paul Mackenzie huko Shakahola, wanahabari wamezuiliwa na asasi za kiusalama dhidi ya kunasa matukio katika shamba hio.

Wanahabari kutoka vituo mbalimbali vya habari ndani na nje ya nchi wamekuwa wakikita kambi katika shamba hilo lenye ukubwa wa ekari 800 wakipeperushwa matukio moja kwa moja kuhusu kinachoendelea na haswa idadi ya miili inayofukuliwa na DCI.

Kulingana na taarifa kutoka Shakahola, wanahabari hao walizuiliwa kuendelea kunasa matukio hayo huku wakisema kuwa polisi hawakutoa sababu yoyote ya kuchukuliwa kwa hatua hiyo.

Maafisa wa polisi walisema ardhi hiyo - ambapo polisi tangu Ijumaa, Aprili 21, wamefukua zaidi ya miili 90 iliyozikwa kwenye makaburi ya kina kifupi - ni eneo lenye misukosuko na eneo la operesheni.

Haya yanajiri baada ya Waziri wa Mambo ya Ndani Kithure Kindiki kutangaza kuwa eneo la uhalifu.

Maagizo ya amri ya kutotoka nje pia yametangazwa na Kuchapishwa kwenye Gazeti la Serikali ndani ya eneo lililotajwa kati ya saa 1800 jioni na hadi saa 0600 asubuhi kwa muda wa siku 30. Hakutakuwa na mikusanyiko ya watu wote, maandamano au harakati ama peke yake au kama kikundi wakati wa muda wa kutotoka nje.

Baada ya marufuku hiyo dhidi ya vyombo vya habari, haijulikani mara moja kama asasi za kiusalama zitaendelea kutoa sasisho kuhusu shughuli ya ufukuzi au la.