Furaha kwa mrengo wa Sabina Chege msajili wa vyama akimpiga kumbo Uhuru Kenyatta

Uamuzi huo unamaanisha kuwa Kioni na Murathe si wanachama tena wa Jubilee.

Muhtasari

• Hatua hiyo sasa inamaanisha kuwa Rais msataafu Uhuru amepoteza chama hicho kwa waasi wanaomuunga mkono Rais Ruto.

• Pia ofisi hio iliidhinisha kusimamishwa kazi kwa mweka hazina wa chama hicho Kagwe Gichohi.

Aliyekuwa Mbunge wa Gatanga David Murathe pamoja na Aliyekuwa Mbunge wa Ndaragwa Jeremiah Kioni.
Aliyekuwa Mbunge wa Gatanga David Murathe pamoja na Aliyekuwa Mbunge wa Ndaragwa Jeremiah Kioni.

Ofisi ya msajili wa vyama vya kisiasa imethibitisha kuondolewa kwenye sajili ya chama cha Jubilee kwa waliokuwa wandani wa Rais mstaafu Uhuru Kenyatta.

Katika uamuzi huo, Msajili wa vyama vya kisiasa Anne Nderitu alisema chama hicho kilifuata utaratibu ufaao kuwatimua katibu mkuu wa chama hicho Jeremiah Kioni na naibu mwenyekiti David Murathe.

Pia ofisi hio iliidhinisha kusimamishwa kazi kwa mweka hazina wa chama hicho Kagwe Gichohi.

Hatua hiyo sasa inawakabidhi washirika wa Rais William Ruto wakiongozwa na kaimu katibu mkuu Kanini Kega uongozi wa chama hicho.

“Kufuatia ukaguzi wa makaratasi yaliyowasilishwa, kwa mujibu wa PPA na katiba ya chama, afisi hii imeridhika kwamba chama kilifuata utaratibu uliowekwa,” aliandika Nderitu katika barua ya tarehe 19, Mei.

"Kwa hiyo, kwa mujibu wa kifungu cha 34 cha PPA, ofisi hii imeboresha rekodi zake na sajili la wanachama wa chama hii."

Uamuzi huo unamaanisha kuwa Kioni na Murathe si wanachama tena wa Jubilee na kwa hivyo hawatakuwa na mamlaka yoyote kwenye chama.

Upande huo wa Kega ulifanya kikao cha baraza kuu la uongozi wa taifa wa chama hicho Mei 19 na kupitisha mapendekezo ya Kamati ya Nidhamu ya Chama kuwafukuza Kioni na Murathe kwenye chama.

Maamuzi ya kikao hicho, inayoungwa mkono na naibu katibu mkuu Joshua Kutuny, iliiandikia ofisi ya msajili wa vyama kuwasilisha maazimio hayo ya Mei 19.

Hatua hiyo sasa inamaanisha kuwa Rais msataafu Uhuru amepoteza chama hicho kwa waasi wanaomuunga mkono Rais Ruto.

Pia ina maana kwamba Kongamano la Kitaifa la Wajumbe iliyofanyika siku ya Jumatatu na kuongozwa na Rais msataafu Uhuru Kenyatta hauna maana yoyote na kwamba maazimio yaliyotolewa huenda yasiwe na athari yoyote kisheria.