Mfuasi sugu wa Raila, Gaucho akamatwa tena

Sababu ya kukamatwa kwake bado haijajulikana.

Muhtasari

• Ni mara ya pili ndani ya wiki moja kumkamata Gaucho, Mfuasi mkubwa wa  kiongozi wa muungano wa Azimio la Umoja One Kenya Raila Odinga.

• Waziri wa zamani, Eugine Wamalwa aliapa kuhakikisha kuwa Gaucho anaachiliwa.

Rais wa Bunge la Wananchi Calvin Okoth almaarufu Gaucho akizungumza wakati wa Kongamano la wajumbe wa Jubilee Mei 22, 2023.
Rais wa Bunge la Wananchi Calvin Okoth almaarufu Gaucho akizungumza wakati wa Kongamano la wajumbe wa Jubilee Mei 22, 2023.
Image: MAKTABA

Calvin Okoth almaarufu Gaucho amekamatwa nje ya City Hall baada ya juhudi za polisi kumtafuta tangu Jumamosi terehe 27, Mei.

Sababu ya kukamatwa kwake bado haijajulikana.

Siku ya Jumatatu, Gaucho alikuwa amefika nje ya City Hall na alikuwa akipiga gumzo na wafuasi wake wakati polisi watatu  walipofika na kuamrisha  aandamane nao.

Maafisa hao walimpeleka kwenye Subaru ya bluu iliyokuwa ikingoja na kuondoka kwa kasi.

Ni mara ya pili ndani ya wiki moja kwa Gaucho kukamatwa, mfuasi mkubwa wa  kiongozi wa muungano wa Azimio la Umoja One Kenya Raila Odinga.

Wiki iliyopita, alikamatwa na kuzuiliwa usiku kucha katika kituo cha polisi cha Muthangari kabla ya kuachiliwa bila kufunguliwa mashtaka yoyote kufuatia kukamatwa kwake Mei 23.

Kiongozi huyo wa Bunge la Wanaanchi alishangaa ni kwa nini polisi walimkamata alipokuwa akielekea katika ofisi za Nation Media Group kwa mahojiano. Alipinga hatua hiyo akiitaja kuwa ni unyanyasaji.

“Nilienda Central kuchukua simu zangu ambazo zilichukuliwa mara ya mwisho nilipokamatwa. Lakini nilipoingia katika moja ya ofisi hizo, maofisa hao walisema kuna watu fulani wananitafuta. Mwanzoni, nilifikiri ni mzaha lakini baadaye watu saba walikuja na kunichukua wakisema wananitafuta.”

“Walichukua simu yangu kabla sijampigia Babu Owino na kuizima. Hawajaniambia kwa nini walinikamata.”

Aliyekuwa Waziri wa Ulinzi Eugene Wamalwa alionya serikali kukoma kuwatishia Wakenya.

“Wameanza kuwalenga na kuwakamata wafuasi wa Azimio. Tulikuwa na kijana aliyeitwa Gaucho, ambaye mrithi wangu alisema ni mtu wa hali ya chini na hapaswi kuonekana akiwa na viongozi wakuu. Hawa ndio ‘Hustler’ halisi wanaochukuliwa kimzaha na ‘hustler’  serikalini,” alisema.

Wamalwa alidai kukamatwa kwa Gaucho kulikusudiwa kumtisha baada ya kutoa kauli kali katika Kongamano la Kitaifa la Wajumbe wa Jubilee jijini Nairobi Mei 23, 2023.

Waziri huyo wa zamani aliapa kuhakikisha kuwa Gaucho anaachiliwa bila masharti.