Sahau kuhusu maendeleo ikiwa unapinga Mswada wa Fedha - Gachagua kwa wabunge

"Kama mbunge wenyu anasema watu wasilipe kodi, asiulize barabara kwa sababu itatoka wapi?" Gachagua alisema.

Muhtasari

• Gachagua alisema baadhi ya viongozi wanawaambia Wakenya kukataa Mswada wa Fedha ilhali wanataka huduma kutoka kwa serikali.

• Mswada huo ambao tayari uko katika Bunge la Kitaifa ukisubiri uamuzi wa wabunge, umekuwa ukishutumiwa vikali na viongozi na Wakenya kwa pamoja.

Image: DP Rigathi Gachagua

Naibu Rais Rigathi Gachagua amewaonya Wabunge watakaopinga mswada wa fedha kuwa wasiulizie maendeleo ya barabara katika eneo bunge zao.

Akiongea Jumapili wakati wa Ibada ya Kutoa Shukrani huko Narok, Gachagua alisema wabunge wanaopinga Mswada wa Fedha hawafai kuomba maendeleo katika maeneo yao.

Gachagua alisema baadhi ya viongozi wanawaambia Wakenya kukataa Mswada wa Fedha ilhali wanataka huduma kutoka kwa serikali.

"Kama mbunge wenyu anasema watu wasilipe kodi, asiulize barabara kwa sababu itatoka wapi?" Gachagua alisema.

Awali Gachagu alipokuwa Kitui mbunge mmoja kutoka eneo hilo katika hotuba yake mbele ya Naibu wa Rais aliwaambia wakazi kukataa Mswada wa Fedha wa 2023.

Gachagua aliwauliza wakazi kwa nini mbunge huyo atasema hivyo na bado atarajie kufadhiliwa kwa miradi ya barabara na hospitali.

Mswada huo ambao tayari uko katika Bunge la Kitaifa ukisubiri uamuzi wa wabunge, umekuwa ukishutumiwa vikali na viongozi na Wakenya kwa pamoja.

Akiongea katika hafla hiyo, Ruto alisema anasubiri kuona wabunge ambao watapinga mswada huo.

“Nasubiri Wabunge ambao watakwenda kupiga kura ya kupinga ajira kwa vijana hawa, dhidi ya ujenzi wa makazi ambayo yangewapa nafasi watu hawa kumiliki nyumba yenye mkopo wa asilimia tano,” Rais Ruto alisema.

Alisema wabunge walikuwa na mikopo ya asilimia ya chini kwa sababu ya ushuru unaolipwa na Wakenya.

Ruto alitoa wito kwa wabunge wa Kenya Kwanza kuipitisha mswada huo huku kiongozi wa upinzani Raila Odinga akiwataka wabunge wa Azimio kuipinga.

Mswada huo unapendekeza, miongoni mwa mambo mengine, kwamba wafanyakazi wachangie asilimia tatu kwenye hazina ya Nyumba.

Hii, Ruto alisema, sio ushuru bali ni mchango na mpango wa kuwasaidia maskini kumiliki nyumba katika mradi wa nyumba za bei nafuu.

Aliongeza kuwa ikiwa mswada huo utapitishwa mchango huo utakuwa ni wa lazima.