Ole Sapit ataka serikali kuruhusu wakenya kupata watoto wasiozi wanne

Sapit alisema ni makosa kushinikiza Wakenya kupata watoto wengi huku kukiwa na hali mbaya ya kiuchumi.

Muhtasari

• Alisisitiza umuhimu wa kupanga uzazi ili kupunguza shinikizo kwa uchumi na kuongeza idadi ya Wakenya wanaolipa zaka na ushuru.

• "Kama nchi, tuna idadi kubwa ya vizazi vya vijana kutoka kwa watoto wachanga hadi chuo kikuu. Wanategemea sana na hawana tija na bajeti inakwenda kudumisha idadi hii ya watu huku serikali ikitumia rasilimali nyingi katika afya na elimu,”

Askofu Mkuu Jackson Ole Sapit ameiomba serikali kuzingatia kuweka kikomo cha idadi ya watoto kwa kila familia ili kupunguza shinikizo katika uchumi’.

Kasisi huyo alitofautiana na baadhi ya viongozi wa kisiasa waliowashauri Wakenya kupata watoto zaidi.

Alisisitiza umuhimu wa kupanga uzazi ili kupunguza shinikizo kwa uchumi na kuongeza idadi ya Wakenya wanaolipa zaka na ushuru.

"Kama nchi, tuna idadi kubwa ya vizazi vya vijana kutoka kwa watoto wachanga hadi chuo kikuu. Wanategemea sana na hawana tija na bajeti inakwenda kudumisha idadi hii ya watu huku serikali ikitumia rasilimali nyingi katika afya na elimu,” alisema.

Sapit alisema ingawa ni kwa manufaa ya viongozi hao wa kisiasa kuwa na idadi zaidi, ni makosa kushinikiza Wakenya kupata watoto wengi huku kukiwa na hali mbaya ya kiuchumi.

"Najua Mkuu wa Nchi anachoma mafuta ya usiku wa manane ili kuboresha uchumi lakini lazima tukubali kwamba vijana wengi hawana ajira na serikali inatumia pesa nyingi kwa idadi ya vijana. Tulikuwa tunamsikiliza (waziri wa zamani) Ole Ntimama akituambia tuzae watoto zaidi na mimi mwenyewe nina saba lakini nadhani tuanzishe kampeni ya kuwaambia Wakenya kupunguza idadi ya watoto hadi 4,” alisema Ole Sapit.

Alisema haya  wakati wa sherehe za kianglikana dayosisi ya Eldoret wakati dayosisi hiyo inatimiza miaka 40 tangu kuanzishwa kwake. Rais William Ruto alikuwa miongoni mwa watu mashuhuri waliohudhuria.

Seneta wa Nyandarua John Methu alijibu kwa mzaha wito wa Askofu, akisema serikali haifai kutekeleza pendekezo hilo kwani itamnyima fursa ya kupata watoto zaidi.

Dayosisi ya Eldoret ilifunguliwa mwaka wa 1983 huku marehemu Alexander Muge akiwa askofu wake wa kwanza msimamizi.

Magavana Jonathan Bii (Uasin Gishu), Stephen Sang (Nandi), Kenneth Lusaka (Bungoma), Wesley Rotich (Elgeyo Marakwet), Waziri wa Uchukuzi Kipchumba Murkomen na Katibu Mkuu wa chama cha UDA Cleophas Malala waliandamana na Rais.