Serikali itaendelea kutoza ushuru wa Nyumba za bei nafuu - CS Alice Wahome asisitiza

Waziri Wahome sasa anasema kuwa waajiri wataendelea kutuma mchango wao wa asilimia 1.5 pamoja na kiwango sawia kwa wafanyikazi wao.

Muhtasari

• Wahome aliwasisitiza waajiri wote kuendelea kukata na kuwasilisha ushuru hadi tarehe iliyowekwa.

• Uamuzi wa Mahakama ya Juu ulikuja kama kikwazo kisichotarajiwa kwa Rais William Ruto kwani ametangaza mpango wa Makazi kama nguzo kuu ya utawala wake.

WAZIRI ALICE WAHOME
Image: TWITTER

Waziri wa ardhi na maendeleo ya miji Alice Wahome ameweka wazi msimamo wa serikali kuhusu kesi iliyopo mahakamani ya kutaka kuzuia serikali kuacha kutoza ushuru wa ujenzi wa nyumba za bei nafuu.

Waziri huyo alisema kwamba Wakenya wanaolipwa mishahara wataendelea kutozwa Ushuru wa Nyumba ambao unazozaniwa kwani serikali imeshikilia kuwa wataendelea kukusanya makato hayo hadi Januari 10, 2024.

Wahome aliwasisitiza waajiri wote kuendelea kukata na kuwasilisha ushuru hadi tarehe iliyowekwa.

Haya yanajiri kufuatia uamuzi wa Mahakama Kuu siku ya Jumanne ambao ulitoa amri za kusimamishwa kwa utekelezwaji wa kukatwa ushuru wa nyumba za bei nafuu hadi Januari 10.

Uamuzi uliotolewa na jopo la majaji watatu ambao ni Majaji David Majanja, Lawrence Mugambi na Christine Meoli ulitangaza ushuru huo kuwa kinyume na katiba kwa vile ulilenga wafanyikazi wanaolipwa mishahara pekee na hivyo serikali ikapewa muda wa kukaa kwa siku 45.

Wahojiwa, wakiongozwa na wakili George Murugara, walidai kuwa ombi la kuzuiwa kwa amri hiyo litaruhusu serikali kuweka mambo yao sawa.

"Sababu ni kwamba, kwanza, inabidi tufanye marekebisho yanayohitajika kwa utaratibu wa serikali wa kutoza ushuru ili hakuna chama/mkono wa serikali unaoshitakiwa kwa kudharauliwa," Murugara aliiambia mahakama.

Ushuru huo ambao ni nguzo kuu katika Sheria ya Fedha, ulianza kukatwa kutoka kwa Wakenya walioajiriwa mnamo Julai, huku Mamlaka ya Ushuru ya Kenya (KRA) ikiidhinishwa kuwa wakala wa kukusanya.

Waziri Wahome sasa anasema kuwa waajiri wataendelea kutuma mchango wao wa asilimia 1.5 pamoja na kiwango sawia kwa wafanyikazi wao.

Uamuzi wa Mahakama ya Juu ulikuja kama kikwazo kisichotarajiwa kwa Rais William Ruto kwani ametangaza mpango wa Makazi kama nguzo kuu ya utawala wake.

Ruto alikaribisha uamuzi huo, na kuahidi kuwa ataheshimu uamuzi wa mahakama.

Naibu Rais Rigathi Gachagua aidha ameitaka Idara ya Mahakama kuzingatia athari pana kwa jamii kutokana na uamuzi wake huo, akisema kwamba ushuru huo unawezesha serikali kujenga nyumba kwa wingi ili kupunguza uhaba wa makazi nchini Kenya.